Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete, amewataka watumishi wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuongeza nguvu katika kusajili waajiri.
Pia kuhakikisha kwamba wanawasilisha michango ya watumishi wao kwa wakati ili kuwezesha watumishi hao kupata haki yao kwa wakati endapo watapata ajali, kuumia, ugonjwa au kifo kutokana na kazi zao.
Ridhiwani ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi baina yake na watumishi wa WCF kwa lengo la kujadili na kuelekezana namna bora ya kuboresha utendaji kazi.

“Natambua kuwa hadi sasa WCF imesajili asilimia 93.7 ya waajiri wote nchini, lakini hiyo haitoshi na ninaitaka menejimenti ihakikishe kwamba waajiri wote wanasajiliwa hadi kufikia asilimia 100 na wanawasilisha michango yao kwa wakati.
“Na katika hili ninawahimiza watumishi wote muwajibike kutekeleza jambo hili, kwa kuwa ndio msingi mkuu utakaosaidia kulipa fidia kwa wafanyakazi watakaopata ugonjwa, ajali au kufariki wakati wakitekeleza majukumu ya kazi,”amesema.
Ridhiwani pia ameiagiza Menejimenti ya WCF kuhakikisha inafanya uwekezaji katika maeneo yenye tija yatakayosaidia kuuongezea Mfuko uwezo wa kumudu kulipa fidia hususani katika maeneo ya hatifungani ambayo ni salama zaidi.
“Uwekezaji ni sehemu ya jukumu muhimu la WCF, na ili kuhakikisha eneo hili linakuwa na tija, basi mnapofikiria njia ya uwekezaji fikirieni maeneo yaliyo salama ili kuuwezesha Mfuko kumudu jukumu lake la msingi ambalo ni kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaopata madhila kazini,’’ amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema kuwa Menejimenti imepokea maelekezo ya Waziri Ridhiwani na kwamba watumishi wataongeza kasi ya uwajibikaji ili kutekeleza maagizo hayo.
“Tumepokea maelekezo ya Mheshimiwa Waziri ambaye ametutaka kuongeza kasi katika usajili wa waajiri na ukusanyaji wa michango, jambo hili tumelipokea na tutalifanyia kazi,’’ amesema Dkt. Mduma.
Akitoa salamu za shukrani mwakilishi wa wafanyakazi wa WCF, Musa Mwambujule amemshukuru Waziri Ridhiwani kwa kutembelea na kuwasilkiliza wafanyakazi, jambo ambalo limeonesha serikali inavyothamini 
