Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MKURUGENZI Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, ametoa wito kwa wazalishaji na waagizaji wa mbolea nchini kuhakikisha wanazalisha au kuingiza mbolea inayoendana na mahitaji halisi ya udongo ili kuongeza tija ya uzalishaji katika sekta ya kilimo.
Laurent ametoa wito huo katika banda la TFRA, katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara naarufu kama Sabasaba yanayoendelea Dar es Salaam.

Amesema pamoja na ongezeko kubwa la matumizi ya mbolea kutoka tani 360,000 mwaka 2022/2023 hadi kufikia takribani tani milioni moja mwaka 2024, bado ipo haja ya kuwa na mbolea sahihi kwa matumizi sahihi.
Amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inaendelea kupima afya ya udongo nchi nzima, hivyo ni muhimu mbolea iwe na viwango na viambata vinavyolingana na matokeo ya vipimo hivyo.
“Kama taifa, tunategemea hadi mwaka 2030 matumizi ya mbolea yafikie mara mbili ya kiwango cha sasa. Hii ni fursa kubwa kwa wawekezaji kuzalisha au kuagiza mbolea kwa ubora unaoendana na mahitaji ya udongo,” amesema.

Amesema mamlaka hiyo imetoa fursa kwa Watanzania kujihusisha na biashara ya mbolea katika nyanja mbalimbali ikiwemo uzalishaji, uagizaji, uhifadhi, na ufungashaji.
Ametoa mfano wa uzinduzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea kilichopo Nala, Dodoma ambacho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka, pamoja na kiwanda cha Minjingu chenye uwezo wa kuzalisha tani 250,000 kwa mwaka.
Mbali na uzalishaji, amesisitiza pia juu ya uwepo wa fursa za kuhifadhi mbolea, ambapo alihimiza Watanzania kuwekeza katika ujenzi wa maghala ili kusaidia mnyororo wa usambazaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa wakulima.

Amesema mbolea inahitaji kuhifadhiwa kwa viwango maalum kabla ya kumfikia mkulima, jambo ambalo linaweza kuwa chanzo cha kipato kwa wananchi wa kawaida.
Kuhusu ufungashaji, Laurent amesema kuwa fursa katika eneo hilo zinaongezeka, huku akieleza kuwa sasa kuna mahitaji ya vifungashio vidogo vya kilo tano hadi 10 ili kuwafikia wakulima wadogo.
Amesema kwa sasa kuna viwanda vichache vya kufungasha, hivyo kuna nafasi kubwa kwa wajasiriamali kuwekeza katika sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, TFRA imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa uuzaji na usambazaji wa mbolea za ruzuku, ambapo Laurent ametoa wito kwa wakulima kuhakikisha wamejisajili katika mfumo huo ili kupata mbolea kwa bei nafuu.
Amesema mfumo huo sasa umeboreshwa na umeanza kujumuisha pia mbegu za ruzuku na pembejeo nyingine, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa pembejeo bora kwa wakulima.
TFRA ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa lengo la kusimamia ubora na usambazaji wa mbolea nchini ili kuhakikisha wakulima wanapata bidhaa bora kwa ajili ya kuongeza tija katika kilimo – sekta ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.