Pia Waajiri Watakiwa Kufanya Kazi Kwa Karibu Na Watumishi Kuepusha Migogoro
Na James Kamala, Ofisa Habari, Halmashauri ya Mji Nzega.
Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deus Sangu amewataka watumishi wa umma kuwa wabunifu na kufanya kazi kwa bidii katika kuwahudumia wananchi ili kuleta tija kwa maendeleo ya taifa.
Aidha amewataka waajiri wote katika utumishi wa umma kuhakikisha wanafanya kazi kwa karibu na watumishi ili kuepusha migogoro isiyo na tija kwenye utumishi wa umma.
Sangu ameyasema hayo wakati akisikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani Tabora.
“Watumishi wa umma mnapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia nidhamu, ubunifu, kuboresha na kutathmini utendaji wenu ili wananchi waweze kupata matokeo chanya kwenye huduma wanazopatiwa,” amesema.

Amesema serikali imekuwa ikitenga na kutuma fedha za miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na miundombinu, hivyo watumishi wa umma wanapaswa kuendana na kasi hiyo.
Kuhusu upungufu wa watumishi katika Halmashauri ya Mji wa Nzega na Mkoa wa Tabora, Sangu amesema tatizo hilo tayari limepatiwa ufumbuzi kwani mchakato wa kuajiri watumishi tayari umeanza.
“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa vibali vya ajira mpya zaidi ya elfu arobaini na saba na tayari Mkoa wa Tabora unatarajia kupata watumishi wapya zaidi ya 4,000, tukianza na kada za afya,” amesema.
Kuhusu upandishaji wa vyeo kwa watumishi wa umma, Naibu Waziri huyo amesema kuwa serikali imekwisha tenga fedha za kutosha kwa ajili ya mchakato huo, ikiwemo pia fedha za kulipa madeni mbalimbali kama vile malimbikizo ya mishahara ya watumishi.
Wakati huohuo, Sangu amewaasa waajiri kuhakikisha wanatoa mafunzo ya awali kazini kwa watumishi wapya ili waweze kujua wajibu wao na haki zao, na hivyo kuepusha migogoro kazini na mashauri ya kinidhamu katika maeneo ya kazi.
“Wajulisheni na kuwaelekeza mazingira ya kazi, kanuni, na sheria za utumishi wa umma ili waweze kufanya kazi kwa uhuru na amani yenye tija kwa utendaji uliotukuka,” amesema.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai, Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya hiyo Ricardo Komanya, pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega, Leah Kibaki, na watumishi kutoka Idara na Vitengo mbalimbali katika Halmashauri hiyo.