Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WATAFITI kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa mkoani Iringa, wamefanikiwa kuibua mbinu mpya ya kudhibiti mdudu kantangaze ambaye ni adui mkubwa wa zao la nyanya kwa kutumia njia isiyo ya kemikali.
Mhadhiri Mwandamizi wa Kemia chuoni hapo, Dkt. Juma Mmongonyo ameeleza hayo alipozungumza na Mwandishi wa Mfanyakazi katika Banda la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Mhadhiri huyo amesema wakiwa kama timu wameweza kufanya utafiti na kufanikiwa kwa asilimia kubwa
kumdhibiti mdudu huyo, ambaye amekuwa tatizo kubwa kwa wakulima wa nyanya nchini.
Amesema mdudu kantangaze husababisha hasara kubwa kwa wakulima, kiasi cha kulazimika kutumia viuatilifu kila wiki kwa muda wa hadi miezi sita ili kuokoa mazao yao.
Amesema hali hiyo si tu inawagharimu wakulima fedha nyingi, bali pia ina athari za kiafya kwa walaji kwa kuwa mabaki ya viuatilifu hubakia kwenye nyanya, pamoja na uharibifu wa mazingira.
Amesema katika utafiti huo uliofanyika Iringa kwa kushirikiana na wakulima mashambani, watafiti wamegundua dawa mbadala iitwayo SPLAT yenye uwezo mkubwa wa kumdhibiti mdudu kantangaze kwa kutumia mfumo wa kuvutia na kuua madume ya mdudu huyo.
Kwa mujibu wa Dkt. Mmongoyo, dawa hiyo ina harufu inayofanana na ile ya kantangaze jike, hivyo humvutia dume ambaye huja akidhani amepata mwenza, lakini badala yake huangamia.
“Kwa njia hii, tunakata mzunguko wa uzalishaji wa wadudu, kwani madume yanapokosekana, majike hayatapata wenza wa kuzaliana nao,” amesema.
Amesema matokeo ya awali yanaonesha kuwa matumizi ya SPLAT huweza kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya kantangaze mashambani ndani ya kipindi cha wiki tatu, ikilinganishwa na utumiaji wa viuatilifu kila wiki kwa miezi sita.
Amesema mbinu hiyo si tu inawalinda walaji dhidi ya mabaki ya sumu kwenye vyakula bali pia inampunguzia mkulima mzigo wa gharama za kununua dawa kila wiki.
Aidha, inahakikisha nyanya zinazozalishwa zinakuwa safi na bora zaidi, na hivyo zina nafasi ya kukubalika kwenye soko la kimataifa linalohitaji viwango vya juu vya usalama wa chakula.
“Tulianza kufuatilia matokeo ya matumizi ya dawa hii Januari hadi sasa Julai, na tumefurahishwa sana na mafanikio yake.
“Tumeanza maandalizi ya awamu ya pili ya utafiti kwa kipindi cha kiangazi,” amesema.