Novemba 15, mwaka 2023, tukio la kihistoria lilifanyika katika Chuo Kikuu cha Ardhi kwa uzinduzi mkubwa wa Warsha ya Lu Ban.
Na Mwandishi Wetu
Mradi wa Warsha ya Luban umefungua ukurasa mpya katika elimu ya ufundi stadi barani Afrika, ukiwalenga vijana kwa kuwapa ujuzi unaohitajika moja kwa moja kwenye soko la ajira.
Huu ni mpango wa pamoja kati ya China na nchi za Afrika chini ya mwavuli wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Warsha hii imebuniwa kwa lengo la Kukuza stadi za vijana, kuendeleza walimu wa elimu ya ufundi na kuunganisha elimu ya vitendo na mahitaji ya viwanda

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania, Profesa Adolf Mkenda (wa kwanza kulia), Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian (katikati), na maofisa wengine watembelea Warsha ya Luban katika Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam, Tanzania, Novemba 15, 2023.
Jina la warsha linatokana na Lu Ban, fundi maarufu na mbunifu wa kale kutoka China, ambaye sasa jina lake linatumika kuashiria umahiri, ustadi, na bidii kazini.
Mnamo Novemba 2023, Warsha ya Luban ilizinduliwa rasmi nchini Tanzania, kwenye Chuo Kikuu cha Ardhi, Dar es Salaam, baada ya maandalizi ya muda mrefu na ushirikiano wa karibu kati ya wadau kutoka pande zote mbili.
Warsha hii sasa inafanya kazi rasmi, ikiwa ni miongoni mwa warsha chache barani Afrika zilizoanzishwa kwa kuzingatia mazingira halisi ya nchi husika.
Miundombinu ya mafunzo ya Warsha ya Luban imejengwa chuoni na katika bustani ya viwanda ya China-Tanzania, ikiwa na vifaa vya kisasa kama zana za upimaji wa ujenzi, maabara za uhalisia pepe pamoja na Vifaa vya ukarabati wa magari

Wanafunzi wakitumia kompyuta katika Warsha ya Luban katika Chuo Kikuu cha Ardhi jijini Dar es Salaam, Tanzania, Novemba 15, 2023.
Mafunzo hutolewa kwa njia ya mtandaoni na ana kwa ana, yakisisitiza ushirikiano kati ya vyuo na makampuni ili kuhakikisha wanafunzi wanapata uzoefu wa kazi halisi.
Warsha hii imeundwa kwa kuzingatia mahitaji ya Tanzania, huku ikitumia maarifa na teknolojia kutoka China. Walimu wa Tanzania hupokea mafunzo ya kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa Kichina mara kwa mara ili kuboresha ubora wa ufundishaji.
Tofauti na mafunzo mafupi ya muda mfupi, warsha hii pia hushirikiana na vyuo vikuu kutoa elimu ya shahada, hivyo kutoa matokeo ya kudumu na yanayotambulika kitaifa na kimataifa.
Takwimu zinaonesha kuwa Warsha ya Luban nchini Tanzania tayari imewafundisha maelfu ya vijana katika nyanja mbalimbali.
Mpango uliopo ni kufundisha hadi wataalamu 100,000, hasa kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya bustani ya viwanda ya China-Tanzania na pia kushiriki katika mpango mkubwa wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” wa China.
Wahitimu wa warsha hii wameeleza kuridhishwa kwao na mtaala wa vitendo na vifaa vya kisasa, wakisema vimewaongezea uwezo wa kupata ajira bora.
Mradi huu umewezeshwa kwa kiasi kikubwa na usaidizi kutoka kwa viongozi wa Tanzania na China. Kupitia FOCAC na mipango ya maendeleo ya serikali ya China, Warsha ya Luban zimepewa kipaumbele kama njia ya kuinua elimu ya ufundi na mafunzo ya stadi barani Afrika.
Tanzania siyo nchi pekee yenye warsha hii. Tangu uzinduzi wa kwanza nchini Djibouti mwaka 2019, warsha za Luban zimeanzishwa pia katika nchi kama Kenya, Afrika Kusini, Nigeria, Misri, Uganda, Mali, Madagascar, Ethiopia, na Côte d’Ivoire, kila moja ikijikita katika maeneo yenye umuhimu maalum kwa nchi husika kama vile ujenzi wa miundombinu, uzalishaji wa nishati, na teknolojia ya kisasa.
Warsha ya Luban ni mfano halisi wa ushirikiano wa kimataifa unaoleta matokeo ya moja kwa moja kwa vijana wa Tanzania.
Kwa kuongezeka kwa walimu wa ndani na kuboreshwa kwa mitaala, kuna matumaini makubwa kwamba mradi huu utaendelea kusaidia vijana kupata ujuzi wa kiufundi na ajira zenye tija.
Mwandishi Yu Minghong kutoka Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing, China