Na Lucy Ngowi
MBEYA: ZAIDI ya wanawake 1,000 kutoka mkoa wa Mbeya wamehitimu mafunzo ya muda mfupi ya ujuzi kupitia programu maalum ya ‘Wanawake na Samia’ iliyoanzishwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuwawezesha wanawake kiuchumi na kijamii.
Akizungumza wakati wa mahafali hayo, Mkuu wa Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Mbeya, Hassan Kalima, amesema zaidi ya wanawake 1,184 walijiandikisha kwa hiari katika mpango huo, ambapo 1,063 kati yao waliweza kuhitimu kwa mafanikio makubwa.
Kalima amesema mafunzo hayo yaliyoanza rasmi Julai 15 Julai 2025 na kukamilika Septemba tisa, mwaka huu 2025, yalitolewa katika Chuo cha VETA Mbeya, yakihusisha kozi mbalimbali.
Ametaja kozi hizo kuwa ni ushonaji nguo, ujasiriamali wa utengenezaji sabuni, batiki, vitafunwa, mapishi, udereva, ufundi magari, ujenzi na zaidi ya kozi 40 fupi zinazotolewa na chuo hicho.
“Tulitarajia idadi ndogo, labda wanawake 200 hadi 300, lakini mwitikio ulikuwa mkubwa sana. Hii inaonesha ni jinsi gani wanawake wanathamini nafasi ya kujifunza ujuzi utakao wasaidia kujitegemea,” amesema Kalima.
Amesema wahitimu walionyesha furaha na shukrani kwa kupatiwa nafasi hiyo adhimu, ambapo kama ishara ya kutambua mchango wa serikali, walimshonea mgeni rasmi vazi la heshima la kitenge kama zawadi.

Kwa upande wake, Hamida Mbogo, Katibu wa kikundi cha ‘Wanawake na Samia’ mkoa wa Mbeya na mmoja wa wahitimu wa mafunzo hayo, amesema,
“Tunamshukuru sana Rais wetu Mama Samia kwa moyo wake wa kuwapigania wanawake. Kupitia VETA, wanawake wengi sasa wana matumaini mapya ya kuinuka kiuchumi na kubadili maisha yao.”
Pia amewahamasisha wanawake wote nchini kuchangamkia fursa hiyo akisisitiza kuwa VETA ipo kila kona ya nchi na inatoa mafunzo bora na ya vitendo yanayobadili maisha.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA Tanzania, Anthony Kasore, amesema kuwa awali mpango huo ulilenga kuwafikia wanawake 3000, lakini kutokana na hamasa kubwa na mafanikio yaliyoshuhudiwa, sasa lengo limeongezwa hadi kufikia wanawake 15,000 nchi nzima.
“Tutafungua milango kwa wananchi wote kuja kutueleza wanahitaji mafunzo gani. Sisi tupo tayari kutoa mafunzo kulingana na mahitaji ya jamii,” amesema Kasore.
Mafunzo hayo yanatoa ujuzi wa moja kwa moja unaoweza kutumika mara moja katika soko la ajira au kuanzisha biashara binafsi. Wanawake waliokuwa hawajui namna ya kuoka keki au kushona nguo sasa wanaweza kufanya hivyo kwa ubora wa hali ya juu, na hivyo kuongeza kipato cha familia na kupunguza utegemezi.