Na Mwandishi Wetu
WAKULIMA wamewaomba watafiti wa Mradi wa Mbinu Shirikishi za Wanafunzi na Wakulima katika Uvumbuzi na Uhaulishaji wa Maarifa na Teknolojia za Kilimo (AGRISPAK), kuwatafutia mbinu za kukabiliana na wadudu aina ya Nzi weupe ambao wanaathiri mazao yao na kusababisha upotevu wa zaidi ya asilimia 70 hadi 80.
Wakulima hao wa Kata ya Nyandira Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro, wameomba hayo katika Mradi wa AGRISPARK unaotekelezwa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA).

Ombi hilo limetolewa na wakulima hao wakati Watafiti kutoka SUA walipokutana nao, kutambua changamoto na mahitaji yao ya maarifa.
Katika kutoa changamoto zao itawasaidia watafiti kuandaa machapisho kwa lugha ya Kiswahili ambayo yatawaongezea maarifa hivyo kuwasaidia kuboresha kilimo chao na kuinua kipato cha kaya hizo zilizo kwenye eneo la mradi huo wa utafiti wa AGRISPARK.
Akizungumza na watafiti hao Mkulima Peregrin Adam kwa niaba ya wakulima wenzake, amesema wadudu hao hivi sasa wamekuwa tishio kwa wakulima shambani na hakuna dawa ambayo kwa sasa inaweza kuwaangamiza kwa kuwa wamekuwa wengi.

Amesema wanapopuliza dawa wanaruka ikiisha wanarudi na kuendelea kushambulia mazao.
“Tumefurahi sana kuwaona watafiti kutoka SUA kuja kututembelea na kujua changamoto zinazotukabili,
“Kusema ukweli kwa sasa changamoto kubwa kwenye Kata hii yote ni hawa wadudu weupe huku tunawaita “Masister” kutokana na weupe wao, hakuna dawa tena inayoweza kuwaua wadudu hawa na wamejaa mashambani,

” Wanashambulia zaidi zao la maharage ambalo ndilo zao letu kubwa la biashara kwenye Kata yetu” amesema Peregrini.
Amesema, “Kiukweli kwa sasa kilimo kimekuwa kigumu sana maana wanashambulia karibu mazao yote ya mbogamboga ambayo ndio tegemeo letu kwa kipato kwa wakulima wote kwenye Kata hii, na wanatupa hasara kati ya asilimia 70 hadi 80 ya mazao yanapotea kutokana na mashambulizi yao”.
Mkulima Adam wa Nyandira ameiomba SUA kupitia kwa watafiti wake kuwasaidia kupata ufumbuzi wa tatizo hilo, ikiwezekana kufikisha kilio hicho kwa serikali na wizara ya Kilimo kuwatafutia ufumbuzi wa wadudu hao ambao wanawapa umasikini wakulima wengi kwa sasa.

“Mkiangalia kwa mazingira yetu huku tunalima mbogamboga msimu wote na tunategemewa sana kwa kuzalisha maharage hasa mabichi kwenda mikoa mbalimbali hasa Dar es salaam na Dodoma lakini kwa sasa uzalishaji wetu umepungua mno kutokana na kuongezeka kwa wadudu hawa hatari wasiosikia dawa ,” amesema.
Kwa upande wake Mtafiti Mkuu mwenza wa mradi wa AGRISPARK Dkt. Nicholous Mwalukasa amesema lengo la kuwatembelea wakulima hao ni kutaka kujua changamoto wanazokabiliana nazo katika kilimo ili waweze kutumia uwepo wa machapisho mbalimbali ya kisayansi yaliyopo kuandaa vitabu vidogo.
Vitabu hivyo vitakuwa na mada mbalimbali ili kutoa elimu ya namna ya kukabiliana na changamoto zao ili kuongeza uzalishaji.
“ Hivi sasa tupo kwenye hatua ya tatu ya mradi ambapo tumekuja kupata maelezo na changamoto zenu ili twende kuwatafutia ufumbuzi wake kupitia tafiti mbalimbali zilizofanyika duniani kote na kwa kutumia wataalamu wa SUA na taasisi zingine na baadae tutatayarisha kwa lugha rahisi ambayo mtaweza kuelewa na kutumia elimu hiyo kutatua changamoto hizi.

“Kwanza niwape pole kwa changamoto mnayokutana nayo kwa wadudu hawa na sisi tumelichukua na tunakwenda kuwatafutia majibu sahihi na ya namna ya kuwakabili wadudu hawa pamoja na changamoto zingine mlizoziainisha,
“Tutaziandaa katika nakala ngumu na nakala laini na kuwaletea ili muweze kupata maarifa hivyo kuendelea kulima kilimo chenye tija na kujikwamua kujipatia maendeleo kupitia kilimo cha mbogamboga mnachokifanya zaidi katika eneo hili,” amesema.
Watafiti hao kutoka SUA kupitia mradi wa AGRISPARK wanatembelea Kata zilizo ndani ya mradi huo kwenye Wilaya ya Mvomero, Manispaa ya Morogoro pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vijijini kwa ajili ya kukutana na wakulima na wafugaji kutambua mahitaji yao ya maarifa yanayoweza kusaidia kuinua uzalishaji kupitia kilimo na mifugo katika mnyororo mzima wa thamni wa mazao na mifugo yao.
Mradi wa AGRISPARK unafadhiliwa na Serikali kupitia SUA, kama maono mapana ya uongozi wa chuo wa kutenga fedha za ndani kwa ajili ya kuwawezesha watafiti wake kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.