Na Lucy Ngowi
DODOMA; MAMLAKA ya. Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), imewaalika wakulima kufika katika banda lao lililopo kwenye maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ili kupata elimu kuhusu mlipuko wa panya katika mashamba yao.
Ofisa kutoka Kituo cha Kitaifa cha Kudhibiti Baa la Panya Tanzania TPHPA, Christina Tewele amesema kati ya aina mbalimbali za panya, panya shamba anapatikana katika maeneo yote nchini ambaye kwa kiasi kikubwa husababisha mlipuko.
Akitolea mfano milipuko ya panya ya hivi karibuni iliyotokea katika mashamba ya wakulima, maeneo ya Kanda ya Ziwa wilaya ya Bariadi na Kishapu, amesema TPHPA imefanikiwa kuidhibiti kwa kutumia sumu baada ya njia nyingine kushindikana.
Amesema panya wanapoingia shambani hufanya uharibifu mkubwa kwa kula mazao yaliyopo hivyo kusababisha hasara kwa mkulima.
“Kuna dalili nyingi ambazo mkulima ataziona shambani zitakazomwashiria kuna mlipuko wa panya katika eneo hilo.
“Kitu cha kwanza ataona mashimo hai ya panya, vinyesi vingi vya panya shambani, pia ataona njia nyingi za panya katika shamba lake, na ukipita usiku unakuta panya wanakatiza mara nyingi.
“Pia kitu kingine ni uharibifu wa ile mimea na mazao yakiwa shambani kwa sababu panya anafanya uharibifu tangu hatua ya kwanza ya kupanda mbegu katika ukuaji,” amesema.
Amesema mahindi yakifanikiwa kuota na kuanza kukomaa, panya ana uwezo wa kulipandia na kulitafuna love.
Amesema panya ana uwezo wa kufanya uharibifu wa hadi asilimia 100, hivyo mkulima anaweza kupanda mbegu kesho yake akakuta zimeliwa mashimo yote yako matupu.
“Wakulima waje banda la TPHPA ni fursa kwao kujifunza , panya wanapomwelemea ajue ni wapi akimbilie ili aendelee kuwa salama,” amesema.
Kwa upande wake mdau wa Kilimo kutoka Benki ya Azania, Gailey Kihungwa ameshukuru kupata elimu ya panya, kwamba anaweza kuleta madhara makubwa kwa mkulima.
“Tunashughulika na wakulima tunafikiri fursa hii itatusaidia kuwapa elimu ya jinsi ya kudhibiti panya ni waharibifu wa mazingira na mazao kwa wakulima,”amesema.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Taifa cha Nasaba za Mimea TPHPA, Dk Mujuni Kabululu amesema wamekuwa wakitoa elimu na huduma mbalimbali, eneo la panya waharibifu limekuwa ni kivutio kwa wakulima.
Amesema katika kipindi hiki kumekuwa na baa kubwa la panya,, ” Na nchi imeshambuliwa sana mwaka huu na uliopita.
“Wataalamu wetu kupitia TPHPA wamefanya kazi katika kupambana na panya, kuhakikisha wanadhibitiwa kwa kuwa wanaleta madhara makubwa sana katika kilimo,”.