Na Mwandishi Wetu
MATIBABU ya wagonjwa wenye maumivu makali mwilini yatafanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kupitia tiba radiolojia itakayoongozwa na Daktari Bingwa Mbobezi wa matibabu hayo duniani Profesa David Prologo kutoka Emory Health Care Marekani.
Taarifa kutoka MNH imeeleza tiba hiyo kuwa ni matibabu ambayo daktari bingwa hutumia teknolojia ya picha za uchunguzi za kumuongoza kufanya uchunguzi au tiba kupitia matundu madogo mwilini bila kufanya upasuaji.
Kupitia taarifa hiyo, Daktari Bingwa Mbobezi wa Tiba Radiolojia MNH, Erick Mbuguje amesema kambi hiyo itahusisha matibabu ya wagonjwa wenye maumivu makali ya aina zote yaliyogawanyika katika makundi makuu mawili, yakiwemo maumivu ya mgongo na maumivu ya sehemu nyingine za mwili.
Dkt. Mbuguje amesema kundi la kwanza ni wagonjwa wenye maumivu makali ya mgongo yasiyosababishwa na saratani ikiwemo pingili zilizosagika, kuvunjika au kupukutika ambapo matibabu ya maumivu hayo hayahusishi upasuaji.
Pia diski zinazokandamiza mishipa ya fahamu hivyo maumivu kusambaa sehemu za miguuni ambayo hayatibiki kwa upasuaji na wagonjwa wenye maumivu yatokanayo na maungio ya pingili.
Amesema kwa wagonjwa wenye maumivu ya mgongo yatokanayo na saratani iliyosababisha kuvunjika kwa pingili au kubana kwa mishipa ya fahamu nao watahudumiwa.
Ametaja kundi la pili kuwa ni wagonjwa wenye maumivu makali ya viungo vingine vya mwili ambayo hayajasababishwa na saratani kwenye magoti, mabega, nyonga ambayo matibabu ya maumivu hayo hayaondolewi kwa njia ya upasuaji na kuongeza kuwa katika kundi hilo wenye maumivu mengine yatokanayo na saratani mbalimbali mfano kongosho nao watanufaika na huduma hiyo.
Huduma hizo zitafanyika Novemba nne hadi 15, 2024 katika Idara ya Radiolojia iliyopo karibu na jengo la Utawala katika hospitali hiyo.
MNH inashirikiana na Taasisi ya ROAD2IR ya nchini Marekani kufanya kambi maalum ya uchunguzi na matibabu kwa wagonjwa hao.