Na Danson Kaijage
DODOMA: MBIO za kuwania nafasi ya ubunge wa Jimbo la Dodoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimeanza rasmi leo, baada ya kutangazwa kwa majina ya wagombea nane waliopitishwa na Kamati Kuu ya chama hicho.
Wagombea hao wameanza kujinadi mbele ya wajumbe wa CCM katika kata mbalimbali za jimbo hilo, leo Julai 30,2025 wakiainisha dira na mikakati yao ya kuleta maendeleo endapo watapata ridhaa.
Wagombea waliopitishwa ni Samwel Malecela, Rashid Mashaka, Pascal Chinyele, Samwel Kisaro, Fatuma Waziri, Robert Mwinje, Rosemary Jairo, na Abdulhabibu Mwanyemba.
Kampeni za ndani zimeanza leo Julai 30, 2025 majira ya saa tatu asubuhi katika Kata ya Chigongwe, ambapo Samwel Malecela aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Wazazi wa CCM Mkoa wa Dodoma na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa aliongoza kwa kujinadi mbele ya wajumbe.
Katika hotuba yake kwa wajumbe, Malecela ameainisha vipaumbele vyake vinavyolenga kutatua kero za msingi zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, akisisitiza dhamira ya utumishi uliotukuka na ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi ya maendeleo.
Licha ya kuonekana kuwa na ushindani mkali, baadhi ya wagombea wamekutana na changamoto kadhaa kutoka kwa wajumbe. Samwel Kisaro, mmoja wa wagombea, amejikuta katika hali ya kujitetea baada ya kuulizwa swali na mjumbe wa Kata, Amos Ndubaha, kuhusu ushiriki wake katika migogoro ya ardhi.
Ndubaha ametaka kufahamu ni kwa namna gani Kisaro ataweza kutatua matatizo ya ardhi ilhali anaendesha kampuni inayojihusisha na upimaji, ununuzi, na uuzaji wa viwanja shughuli ambazo zimewahi kuzua mgogoro katika maeneo mbalimbali ya Dodoma.
Kisaro amekana madai hayo akisema si mhusika wa moja kwa moja katika shughuli hizo, na huenda amechanganywa na mtu mwingine mwenye jina linalofanana.
Jimbo la Dodoma Mjini limekuwa na historia ya kubadilisha wabunge mara kwa mara kila baada ya muhula mmoja. Tangu mwaka 1995, wabunge waliowahi kuliongoza jimbo hilo ni pamoja na Ashimu Sagafu (1995–2005), Ephraim Madeje (2005–2010), David Malole (2010–2015), na Anthony Mavunde (2015–2025), ambaye sasa amehamia katika Jimbo la Mtumba.