Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: WAFUGAJI wasio waaminifu wamekuwa wakiongeza unga, mkojo wa ng’ombe, magadi, mafuta ama maji kwenye maziwa jambo ambalo sio sawa kwa kuwa maziwa huharibika upesi.
Ofisa Jinsia na Lishe kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Ruth Mkope amesema hayo alipokuwa akitoa mada kuhusu maziwa katika semina ya Waandishi wa Habari katika kuelekea kilele cha siku ya Kimataifa ya Maziwa Juni Mosi mwaka huu mkoani Morogoro.
Ruth amesema wafugaji hao wamekuwa wakiongeza vitu hivyo kwenye maziwa wengine wakiongeza maji ili yawe mengi, mafuta ili yaonekane ng’ombe wake ana maziwa mazuri ama unga ili yaonekana mazito jambo ambalo halikubaliki katika tasnia hiyo ya maziwa.
Amesema uongezaji wa vitu hivyo ni kuchocheo cha maziwa kuharibika kwa haraka, ndio maana wananchi wanahamasishwa kutumia maziwa yaliyosindikwa ili kuepuka kuuziwa yaliyochakachuliwa.
Amesema mambo mengine yanayochangia maziwa kuharibika haraka ni pamoja na kiwele cha ng’ombe kuwa kichafu, ama ugonjwa wa kiwele, mkamuaji kuwa mchafu au ana magonjwa ya kuhara, kukohoa, kifua kikuu, kucha ndefu, nywele ndefu, uvutaji sigara pamoja na mazingira yanayomzunguka kuwa machafu.
Ili maziwa yasiharibike haraka amesema mkamuaji anapaswa kuwa msafi, asiyekuwa na vidonda, kukohoa, kupiga chafya au magonjwa ya kuambizwa.
Ili wananchi wapate maziwa salama ambayo hayajachakachuliwa watumie yaliyosindikwa.
Katika hatua nyingine amesema, unywaji wa maziwa unapaswa kupewa msukumo kwa watoto wa shule wenyewe bila kutegemea wafadhili.
“Hii itasaida kuongeza unywaji wa maziwa hivyo kufanya hali ya lishe ya watoto hawa kuwa nzuri na pia kuongeza ari ya wafugaji katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa,” amesema.
Akizungumzia Mchango wa benki hiyo kwa wakulima, Mratibu wa Mradi T13P TADB, Joseph Mabula amesema benki hiyo ilianzishwa kwa ajili ya kuchagiza maendeleo ya sekta ya kilimo nchini katika eneo la mazao, mifugo, uvuvi na misitu.
Pia kuwasaidia wakulima wadogo kuondokana na kilimo cha kujikimu na kuzalisha ziada.
“Majukumu yake ni kuchagiza ukuaji wa sekta ya kilimo, kutoa mikopo katika miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwa ni pamoja na kutoa fedha za gharama nafuu,” amesema.
Semina hiyo ya kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari, imeandaliwa na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) kwa kushirikiana na benki hiyo ya TADB.