Na Lucy Ngowi
ARUSHA: WAFANYABIASHARA wa jengo la biashara la Shirikisho la Vyama vya Wafanyajazi Tanzania (TUCTA), lililopo Arusha wameishukuru serikali kwa kufanikisha uzinduzi wa jengo hilo.

Aidha wamemtakia afya njema na mafanikio, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, katika safari zake za kiuongozi.
Pongezi hizo zimetolewa na wafanyabiashara wa jengo hilo, kupitia mwakilishi wao, Emmanuel Saevie, wakati wa hafla ya uzinduzi wa jengo hilo lililozinduliwa na Ridhiwani, kwa kusema ujio wa waziri huyo ni ishara ya kuthamini juhudi za wafanyabiashara na mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
Pia Saevie amelipongeza shirikisho hilo, kwa maamuzi ya kubadili matumizi ya awali ya jengo hilo na kuligeuza kuwa jengo la kisasa la biashara, jambo ambalo limefungua fursa kwa wafanyabiashara wengi kupata maeneo ya kufanyia shughuli zao kwa tija.

“Tunatoa pongezi za dhati kwa uongozi wa TUCTA kwa uamuzi wao wa kulikarabati jengo hili na kulitumia kwa manufaa ya uchumi. Ni hatua ya mfano kwa taasisi nyingine,” amesema Saevie.
Katika hatua nyingine, Meneja Mkuu wa Wakala wa Uwekezaji wa TUCTA (WDC), Muchunguzi Kabonaki, amepongezwa kwa usimamizi madhubuti uliowezesha jengo hilo kukarabatiwa hadi kuwa na mwonekano mzuri na wa kuvutia.

“Bila upendeleo wowote, tunampongeza meneja Kabonaki kwa moyo wake wa kizalendo na ufuatiliaji wa karibu. Amefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na timu nzima kuhakikisha jengo hili linakuwa la kisasa,” amesema.
Aidha, Saevie ametoa salamu za pongezi kwa wananchi wa Jimbo la Chalinze kwa kumpa ridhaa Ridhiwani Kikwete kugombea ubunge bila kupingwa, akisisitiza kuwa ni ishara ya imani kubwa waliyo nayo kwake.
“Tunamtakia kila la heri katika uchaguzi ujao. Ikiwa itampendeza Mheshimiwa Rais, tunaomba aendelee kumteua Ridhiwani kuendelea na nafasi hiyo ili arudi na kuendeleza yale aliyoanzisha, pindi uchaguzi utakapokamilika” amesema.

Katika hatua nyingine, Wafanyabiashara waliopata nafasi ya kufungua biashara zao katika jengo hilo wametoa ahadi ya kushirikiana kikamilifu na mamlaka za serikali katika kulipa kodi, kufuata taratibu, na kushiriki kwenye maendeleo ya taifa.
“Tumepewa nafasi, sasa ni zamu yetu kuonyesha mfano bora wa uaminifu na ushirikiano na serikali yetu,” amesema Saevie.