Na Lucy Lyatuu
WAZIRI Wa Nchi,Ofisi Ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira,Vijana Na Wenye Ulemavu Ridhiwan Kikwete amewataka Wafanyakazi nchini kushiriki Uchaguzi Mkuu huku wakiendelea kuamini amani na mshikamano wa nchi ni jambo muhimu kuliko yote.
Ridhiwan amesema hayo jijini Arusha wakati akizindua jengo jipya la Kisasa la biashara la TUCTA-OTTU linalomilikiwa na Shirikisho La Vyama Vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

Amewataka viongozi wa Vyama Vya Wafanyakazi nchini kuendelea Kuhimiza na Kufundisha amani ya nchi kwa kuwa hakuna nchi nyingine zaidi ya Tanzania.
“Wafanyakazi wa Tanzania ni wadau muhimu kushiriki uchaguzi,” amesema na kuongeza kuwa anatambua kuwa wapo Wafanyakazi kulingana na nyadhifa zao wamegombea nafasi mbalimbali hivyo anawatia moyo kuendelea kupambana kwa kuwa hata mbuyu ulianza kama mchicha.
Amesema pamoja na waliogombea wapo waliofanikiwa ambapo wanatakiwa kujua kuwa mafanikio yao ni msingi uliojengwa na vyama vyao.

Ridhiwan amewataka kutambua kuwa wanaokuwa katika nafasi mbalimbali za uongozi wasiwasahau wenzao.
” Muendelee kuwashika mkono kama ambavyo serikali ya awamu ya sita inavyotambua ujenzi Wa Nchi ni pamoja na mchango mzuri Wa TUCTA katika kuhakikisha mambo mazuri yanakwenda,” amesema