Na Danson Kaijage
DODOMA: MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ametoa wito kwa Watanzania kuanza kutumia vumbi la nyuki kutokana na faida zake lukuki kiafya, akibainisha kuwa linahusisha virutubisho 99 kwa wakati mmoja, na ni salama kwa matumizi ya binadamu wa rika zote.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu mafanikio ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Dendego alieleza kuwa mkoa wa Singida umeendelea kuimarika katika uzalishaji wa mazao ya nyuki, ikiwemo asali na nta, na sasa umeongeza zao jipya la vumbi la nyuki lenye thamani kubwa kiafya.
“Mwanzoni ilionekana linafaa kwa wanaume pekee, lakini sasa wataalamu wamebaini linawafaa watu wote – watoto, vijana na wazee,” amesemaDendego.
Ameongeza kuwa vumbi hilo linapatikana katika Kijiji cha Nyuki mkoani Singida, na kwamba serikali ya mkoa inaendelea kutoa elimu juu ya matumizi yake ili kuhakikisha linawanufaisha wananchi kiuchumi na kiafya.
Katika taarifa hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa pia aligusia mafanikio ya sekta ya afya ndani ya kipindi cha miaka minne, akisema Singida sasa ina vituo vya afya na hospitali za kisasa zenye vifaa vya hali ya juu.
“Kwa sasa hatulazimiki tena kuwapeleka wagonjwa Dodoma, Mwanza au Dar es Salaam kwa matibabu ya kibingwa. Tuna vifaa na tunaendelea kuwajengea uwezo wataalamu wetu ili wavitumie ipasavyo,” amesema.
Mkoa wa Singida unatajwa kuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa mazao ya nyuki nchini, na sasa kupitia ubunifu na utafiti wa ndani, umeanza kuvuna faida zaidi kupitia zao jipya la vumbi la nyuki – hatua inayolifanya kuwa kitovu kipya cha tiba asilia nchini.