Na Lucy Ngowi
DODOMA: KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, amesema Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imeanza kuchukua nafasi muhimu katika kubadilisha sekta za kilimo, uchumi na biashara kupitia ubunifu unaolenga kutatua changamoto zinazowakabili Watanzania katika maeneo mbalimbali ya maisha.
Profesa Nombo amesema hayo alipotembelea banda la VETA katika maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima Nanenane leo Agosti nane, 2025 mkoani Dodoma.

Amesema taasisi hiyo sasa imejikita katika kutoa mafunzo yenye uhalisia wa mahitaji ya sasa, huku ikileta suluhisho kwa changamoto kama ajira, tija kwenye kilimo na ujasiriamali mdogo na wa kati.
“VETA si mahali pa kujifunza tu ni eneo mahsusi la kupata ujuzi kwa mtu yeyote anayetaka kuboresha maisha yake.
“Mafunzo haya yanawajengea Watanzania uwezo wa kujiajiri, hivyo kupunguza utegemezi wa ajira za Serikali,” amesema.

Amesema kuwekeza katika ujuzi ni hatua madhubuti ya kuwawezesha wananchi kuongeza kipato na kuchangia kwa vitendo katika maendeleo ya taifa.
Amewataka Watanzania kutumia fursa ya mafunzo ya VETA kama njia ya kujiendeleza na kuvuka mipaka ya kifikra kuhusu ajira.
Katika hatua nyingine, Nombo amepongeza Bodi ya VETA kwa juhudi zao za kuendeleza bunifu zenye tija ambazo zinajibu moja kwa moja mahitaji ya jamii.
Amesema ubunifu wa VETA una mchango mkubwa katika kujenga taifa lenye watu wabunifu, wenye ujuzi, na wenye uwezo wa kutatua matatizo kwa njia endelevu.
Kwa sasa, VETA inaendelea kuonesha mwelekeo mpya wa elimu ya ujuzi nchini, ikiweka msingi wa uchumi wa viwanda na maendeleo ya kijamii yanayojengwa juu ya maarifa na ubunifu wa ndani.