Na Lucy Ngowi
DODOMA:MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) imejidhihirisha kuwa chombo muhimu si tu cha kutoa elimu ya ufundi, bali pia cha kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia uzalishaji wa bidhaa na huduma zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa.
Hilo limeonekana katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake.
Mtaalamu wa ubunifu na ujenzi wa majengo kutoka VETA Makao Makuu, Joseph Mchanake, amesema hayo katika banda la mamlaka hiyo katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Amesema mafanikio ya taasisi hiyo ni ushahidi wa dira, dhamira na utekelezaji wa mipango inayozingatia mahitaji halisi ya taifa.
“Leo hii mafundi wanaohitimu kutoka VETA hawajiandai tu kwa soko la ajira, bali pia wanazalisha bidhaa halisi wakati wa mafunzo yao, jambo linalowaweka moja kwa moja kwenye mazingira ya kiuchumi,” amesema Mchanake.
Amesema kupitia tafiti za kila mwaka za soko la ajira, VETA imekuwa ikibaini kwa usahihi aina ya fani, bidhaa na teknolojia zinazohitajika sokoni, hali inayoifanya taasisi hiyo isalie kuwa hai na yenye kuakisi mahitaji ya wakati.
Amesema mwaka 2021, VETA ilikuwa na vyuo 47 nchini kote lakini hadi kufikia mwaka huu, 2025 idadi hiyo imeongezeka hadi vyuo 80, huku serikali ikiendelea na ujenzi wa vyuo vingine 65 — vyuo vya wilaya 64 na chuo kimoja cha mkoa.
“Lengo ni kuhakikisha karibu kila mkazi wa Tanzania anaweza kupata elimu ya ufundi stadi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu,” amesema.
Kwa maelezo yake, kila eneo lina fani zinazolenga kuchakata maliasili na fursa za kipekee za kijiografia na kutolea mfano Kanda ya Ziwa kwamba wanatiloa mafunzo ya zana za uvuvi na uchakataji wa mazao ya samaki.
Mkoani Arusha ni Utalii na huduma za wageni, Mtwara ni Kilimo cha korosho na uzalishaji wa bidhaa zake.
Amesema ushirikiano kati ya VETA na viwanda umekuwa na matokeo makubwa kwa kuwa wafanyakazi wa viwanda hupatiwa mafunzo ya kuongeza ujuzi, huku wanafunzi wa VETA wakipewa nafasi za mafunzo kwa vitendo jambo linalowaandaa vizuri kwa ajira.
Kwenye upande wa sekta ya madini, amesema VETA haina machimbo yake, lakini kwa kushirikiana na sekta hiyo, vijana hupatiwa mafunzo ya kitaaluma ya uchimbaji na uchenjuaji, kisha hupelekwa machimboni kupata uzoefu wa moja kwa moja.
Vile vile amesema, VETA imekuwa mstari wa mbele kurasimisha ujuzi wa mafundi waliopata maarifa kwa njia zisizo rasmi.
“Tunawafuata walipo, tunawapima, tunawapa mafunzo ya ziada kama kunahitajika, kisha tunawapa vyeti vinavyotambulika kisheria,” amesema.
Amesema vyeti hivyo huwasaidia mafundi hao kuomba ajira kwenye taasisi rasmi na kuongeza wigo wa kipato chao.
Kuhusu makundi maalum, amesema kwa kushirikiana na serikali na wahisani, VETA hutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wajasiriamali wadogo na wa kati. Wanawake, wajasiriamali wa samia, mama lishe na makundi maalum kama watu wenye ulemavu pia wamekuwa wakifikiwa kupitia programu maalum.
“Hatuwaoni kama watu wa kusaidiwa bali kama mafundi halali wanaostahili nafasi sawa. Idadi ya wanafunzi wenye ulemavu imeongezeka kutoka nane hadi 362 kwa mwaka,” amesema.
Amesema falsafa ya VETA inaelekeza kuwa ujuzi ni silaha ya kiuchumi. Kila mwanafunzi hufundishwa kujiamini, kuanzisha biashara, kuajiri wengine, au kuwa tayari kwa soko la ajira rasmi.
“Kwa sasa, zaidi ya wanafunzi 83,000 wanadailiwa kila mwaka, ikilinganishwa na wanafunzi 1,940 wa mwanzo. Ongezeko hilo linaendana na ongezeko la vyuo na fani nchini,” amesema.