Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: USAFIRISHAJI mizigo katika reli ya kiwango cha kimataifa (SGR), uko mbioni kuanza baada ya kukamilika kwa majaribio ya mabehewa 264 kati ya 1430 yanayotengenezwa na kampuni ya CRRC ya China.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Fredy Mwanjala imesema kuhusu kukamilika huko kwa majaribio ya mabehewa ya mizigo ya SGR.
Katika taarifa hiyo, Mwanjala amesema mabehewa hayo 264 ya mizigo yaliwasili nchini Disemba mwaka jana 2024.
“Majaribio ya mabehewa hayo yalichukua mwezi mmoja yalifanyika chini ya usimamiziwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA),
“Yalijikita katika maeneo mawili ambayo ni tuli na mwendo. Lengo la majaribio hayo ilikuwa ni kuangalia umadhubuti wa mabehewa treni inapokuwa kwenye mwendo,” amesema.
Amesema wakati wa majaribio hayo LATRA imefanya kaguzi za mabehewa yote 264, kati ya hayo 200 yakiwa ni ya makasha na 64 ni ya mizigo isiyofungwa.
“Aidha LATRA imejiridhisha kuwa ubunifu wa mwendo kasi wa kilomita 120 kwa saa umefikiwa na kuthibitisha kuwa yamefanya vizuri katika mifumo yote muhimu ikiwemo brekina kwenye kona,” amesema.