Lucy Ngowi
DODOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi), Deus Sangu, amesema kuna upungufu mkubwa wa maofisa katika dawati la jinsia nchini, ambapo kwa sasa wapo maofisa wanne tu.
Akizungumza katika Kongamano na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa Jamii Tanzania (TASWO), Sangu amesema serikali inaendelea kukabiliana na changamoto ya upungufu wa wataalamu hao, hususan katika sekta ya elimu.
Aidha, amewataka wataalamu wa ustawi wa jamii kuzingatia maadili ya taaluma yao, akisisitiza kuwa wao ni tegemeo muhimu kwa makundi yenye uhitaji maalum, yakiwemo watoto waliofanyiwa ukatili pamoja na familia zenye migogoro.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuimarisha maadili hayo sambamba na kuhakikisha kunakuwa na usambazaji sawa wa wataalamu wa ustawi wa jamii nchini.
Sangu ameeleza kuwa changamoto hiyo inahitaji ushirikiano wa wizara mbalimbali, ikiwemo Wizara ya Elimu pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto.
Vilevile, amewahimiza wataalamu hao kutumia mifumo ya kielektroniki ili kurahisisha ukusanyaji na usimamizi wa taarifa.
Amebainisha kuwa hadi kufikia mwisho wa mwaka 2025, serikali ilikuwa imeajiri maofisa ustawi wa jamii 1,724, hatua iliyosaidia kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi hadi ngazi ya kata na vituo vya afya.
Hata hivyo, ameeleza kuwepo kwa changamoto ya usambazaji usio sawa wa wataalamu hao, ambapo asilimia 34 wamejikita katika makao makuu, huku zahanati zikiwa na asilimia 4.29 pekee.
Kwa upande mwingine, amesema serikali inaendelea na mchakato wa kuandaa Sheria ya Taaluma ya Ustawi wa Jamii, ambayo inalenga kulinda hadhi ya taaluma hiyo pamoja na kuboresha mazingira ya kazi na maslahi ya wataalamu wake.
Ameongeza kuwa ajira zitaendelea kutolewa kulingana na uwezo wa bajeti, zikilenga zaidi maeneo yenye upungufu mkubwa kama zahanati na kata.
Sangu amewataka wataalamu wa ustawi wa jamii kuimarisha mahusiano ndani ya jamii ili kudumisha amani na utulivu.

