Na Danson Kaijage
DODOMA: WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega, ameridhishwa na ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya Jiji la Dodoma yenye kilomita 112.3, ambayo utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 85.
Ulega amesema hayo wakati akikagua mradi huo ambapo amewaagiza wataalam wa Wakala wa Barabara (TANROADS) kuhakikisha wanawasimamia Makandarasi wa mradi huo kukamilisha kwa wakati na ubora.

“Nimekagua na nimeridhishwa na hatua zilizofikiwa katika awamu zote mbili na malengo ya Serikali ni kuwa mradi huu ukamilike kwa wakati na nimeelekeza wataalam kutoka TANROADS hadi kufikia mwezi Juni wawe wamefika asilimia 90,” amesema.
Pia amesema serikali inatarajia kujenga barabara ya njia nne na sita kuanzia Chamwino Ikulu hadi katikati ya jiji hilo ambapo kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za manunuzi za kumpata mkandarasi.
Katika eneo la Ihumwa amesema serikali ina mpango wa kujenga barabara ya kisasa ya njia za kupishana, ili kuruhusu magari kupita katika mji wa Serikali wa Magufuli na yaendayo mjini bila kuwa na kizuizi chochote.

Vilevile, Waziri Ulega amezungumzia umuhimu wa Taasisi za TANROADS, Shirika la Reli Tanzania (TRC ) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kufanya kazi kwa kushirikiana ili kuwezesha mradi huo wa kimkakati kukamilika kwa wakati.
Katika hatua nyingine amesema ujenzi wa miundombinu ya barabara za juu maeneo ya Morocco na Mwenge jijini Dar es salaam, upo kwenye mpango mzuri, Wizara inaendelea kukamilisha taratibu za kitaalam ili kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.
“Nitumie fursa hii kuwaambia watanzania kwamba bado Serikali inayo mpango wa kuzijenga Flyover za Mwenge na Morocco na hatua iliyopo wataalam wameniambia wanakamilisha taratibu na wafadhili wa mradi JICA hadi kufikia mwezi Julai fedha za mkopo zitakuwa zishasainiwa,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Aloyce Matei amesema hadi kufikia Julai mwaka huu, matarajio yao ni kwamba fedha za mradi wa ujenzi wa barabara za juu za Morocco na Mwenge zitasainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Naye, Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS, Japheson Nnko amemhakikishia Waziri Ulega kuwa watasimamia Makandarasi hao kuhakikisha mradi wa mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma unakamilika kwa ubora na wakati kama ilivyosainiwa kwenye mkataba.
Amebainisha kuwa mradi huo umegawanywa sehemu mbili ambapo Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) anayejenga sehemu ya Nala-Veyula-Mtumba-Ihumwa bandari kavu (km 52.3) anatarajiwa kukamilisha ifikapo mwezi Julai, 2025.
Na Mkandarasi Avic International anayejenga sehemu ya Ihumwa bandari kavu-Matumbulu-Nala (km 60) anatarajiwa kukamilisha ifikapo Agosti, 2025.