Na mwandishi wetu Kilwa Lindi
WAZIRI wa Madini Anthony Mavunde amesema Ujenzi wa kiwanda cha kusafisha madini ya chumvi kinachojengwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika eneo la Lingaula Wilayani Kilwa ni utekelezaji wa ahadi ya serikali kwa wakulima wa chumvi.
Mavunde amesema kwa kueleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara Mkoani Lindi alisema hayo, hivyo utekelezaji wake umeanza.
Ameyasema hayo alipotembelea eneo litakapojengwa kiwanda hicho ikiwa ni pamoja na kupokea rasmi Hati ya umiliki wa ardhi wa eneo hilo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
“Ninamshukuru Rais Samia kwa kusikia kilio cha wakulima wa chumvi juu ya ukosefu wa masoko ya uhakika, hatua iliyosababisha kutupa maelekezo ya kuhakikisha tunasimamia ujenzi wa kiwanda hiki haraka ili kutatua kero hiyo ya muda mrefu kwa wakulima wa chumvi wa maeneo mengi nchini ikiwemo wa Mkoa wa Lindi.
“Rais alipokuja kwenye ziara yake katika Mkoa huu, moja kati ya mambo aliyoyasikia na kupokea ni kilio cha wazalishaji wa madini ya Chumvi, hivo ameagiza kiwanda cha chumvi kijengwe hapa,.

“Na niwaambie Rais anafuatilia suala hili la wazalishaji wa chumvi na hatua hii ni utekelezaji wa ahadi yake kwenu baada ya kusikia kilio chenu”
“Rais wetu anayodhamira kwa dhati ya kuwanyanyua wazalishaji wa madini ya chumvi ili waweze kupiga hatua, kama ilivyo kwa wachimbaji wa madini mengine nchini,” amesema.
Pia Waziri Mavunde ameiagiza STAMICO kufanya nafunzo ya namna bora ya kulima chumvi ili wazalishe yenye ubora unaofaa kabla ya Disemba mwaka huu.
Sambamba na hilo, Waziri Mavunde ameitaka STAMICO kuangalia uwezekano wa kuingia mikataba ya utatu kati yake, wazalishaji hao wa chumvi pamoja na mabenki ili wazalishaji wawezeshwe kupata mikopo nafuu hatimaye wazalishe chumvi ya kutosheleza uhitaji.
Awali, akitoa taarifa fupi kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO DKt. Venance Mwasse amesema kuwa Chimbuko la Mradi huo ni Maendeleo ya utekelezaji wa mipango ya Shirika pamoja na Maagizo ya Rais Suluhu Hassan aliyeagiza kusaidia wachimbaji wadogo wakiwemo wa chumvi.
Dkt. Mwasse amesema mbali na Kiwanda hicho kuchenjua madini ya chumvi, pia kitakuwa kinatoa Shamba darasa kwa wakulima wa chumvi ili kuwajengea uwezo wa kuzalisha chumvi yenye ubora zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO, Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo alieleza kwamba mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho unataraji kukamilika na kuanza uzalishaji Aprili, mwakani.
Amesema mtambo umeshaagizwa kutoka nchini India na kulipiwa asilimia 50 ya gharama, na unatarajiwa kuwasili Mwezi Oktoba, 2024.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Lindi, Zainab Telack amesema kuwa kukamilika kwa kiwanda hicho kutasaidia kufungua fursa sio tu kwa wakulima wa chumvi, bali kwa wananchi wa mkoa huo.