Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: MAMIA ya wananchi wamejitokeza katika viwanja vya Shule ya Msingi Tabata kuhitimisha kampeni za Chama Cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA).
Bila kujali mvua kubwa iliyonyesha kwa saa mbili mfululizo, wananchi hao wakiwa wamevalia sare za chama hicho na kubeba mabango yenye picha na jumbe mbalimbali za mgombea urais na wagombea ubunge wa majimbo ya Dar es Salaam, walijitokeza kwa wingi kusikiliza hotuba za viongozi wao.

Akizungumza na umati huo, Mgombea Urais wa CHAUMMA, Salum Mwalim, amewataka wananchi kupiga kura ya mabadiliko ili kujikomboa na maisha magumu.
“Twendeni tukapige kura ya mabadiliko ili tuyabadilishe maisha ya watumishi wa umma, wakulima, wafugaji na huduma bora za afya.
“Leo kila sekta inalia maisha magumu, hakuna aliye salama… vijana ndiyo kabisa, wanaomaliza shule hawana ajira wanaishia kuendesha bodaboda na kubeti huku mikeka inachanika,” amesema Mwalim.

Ameongeza kuwa, “Nendeni mkaniamini, mkanichague, nawakalilishia Watanzania amani.”
Mwalim amewashukuru Watanzania kwa kufanya kampeni za utulivu na amani, Jeshi la Polisi kwa kazi ya ulinzi na usalama, Tume ya Uchaguzi (NEC) kwa ushirikiano wao, pamoja na timu yake nzima ya kampeni.

