Na Lucy Lyatuu
TUME ya Taifa ya Mipango imewataka waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ili kuhakikisha wananchi wote wanaitambua, wanaielewa na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.
Wito huo umetolewa Jijini Dar es salaam mapema Agosti 19,2025 na Naibu Katibu Mtendaji wa Tume hiyo anayeshughulikia Mipango ya Kitaifa
Dkt Mursali Milazi wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa habari yalioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu Duniani (UNFPA) kwa kushirikiana na Tume hiyo.
Amesema Vyombo vya habari vina nafasi kubwa ya kuhakikisha kila Mtanzania anapata uelewa sahihi kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.
“Utekelezaji wa Dira hii utaanza rasmi katika mwaka wa fedha 2026/2027…
kutekeleza Dira ni hatua moja, lakini kuwaandaa wananchi na wadau mbalimbali kuelewa na kushiriki utekelezaji wake ni hatua muhimu zaidi.”amesema Dkt Milazi

Amesisitiza kuwa serikali imejipanga kikamilifu kwa ajili ya utekelezaji wa Dira hiyo kwa kuandaa mifumo ya usimamizi na uwajibikaji, ambayo itasimamiwa na Tume ya Mipango ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kwa wakati.
“Dira hii ni ya kwetu sote, hivyo kila Mtanzania anatakiwa aweze kuelewa kwa undani. Mwananchi wa kawaida akiulizwa, mahali popote alipo, awe na majibu ya msingi kuhusu malengo na mwelekeo wa nchi yetu hadi 2050,” ameongeza Dkt Milazi.
Kwa upande wake Msimamizi wa Kitengo cha Idadi ya watu na Maendeleo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Idadi ya watu Duniani (UNFPA) Samweli Msokwa amesema kuwa ushiriki wa vijana, wanawake na makundi maalumu ni muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, ambayo imeandaliwa kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Mipango.
Amesema shirika hilo limekuwa likishirikiana kwa karibu na Serikali katika nyanja mbalimbali, ikiwemo usimamizi wa uzalishaji wa takwimu na data muhimu za maendeleo na kuzisambaza kwa jamii kwa matumizi sahihi ya sera na mipango.
“Katika hatua za awali za maandalizi ya Dira hii, UNFPA ilishirikiana na Serikali kufikisha maudhui ya dira kwa makundi mbalimbali, ikiwemo waandishi wa habari ili kusaidia kufikisha elimu kwa wananchi.”amesema
Na kuongeza kuwa
“Waandishi wa habari ni kundi muhimu katika kuwaelimisha wananchi kuhusu Dira hii. Wananchi ndio watekelezaji wakuu, hivyo elimu yao ni msingi wa mafanikio ya Dira,” amesema Msokwa
Aidha, alisisitiza kuwa vijana wanapaswa kuielewa vyema Dira ya 2050 ili waweze kutambua fursa zilizopo, kujifunza na kuwa sehemu ya mabadiliko ya maendeleo nchini.
