Na Mwandishi Wetu
MOROGORO: SHERIA ya Takwimu imependekezwa ifanyiwe marekebisho ili iendane na mahitaji ya sasa, hali ya maendeleo ya kijamii, kiuchumi, na kisayansi nchini.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania George Mandepo amesena kamisheni imekutana mkoani Morogoro kujadili utekelezaji wa kazi ya mapitio ya Sheria hiyo ya takwimu, ili kuiboresha kuifanya iendane na wakati uliopo .
Amesema sheria hiyo ni muhimu kwa sababu inasimamia uzalishaji, ukusanyaji na usambazaji wa takwimu rasmi nchini ikiwemo takwimu za kiutwala ambazo ni muhimu katika kupanga sera, kutathmini maendeleo, na kufanya maamuzi.
Amesema mapitio ya Sheria hiyo yamejumuisha viini mbalimbali vya utafiti kama vile uhuru wa taasisi katika kuzalisha na kusambaza takwimu ili kuhakikisha takwimu zinazokusanywa zinapatikana kwa urahisi na usahihi kwa watumiaji wote, ikiwemo watafiti, wawekezaji na wananchi.

“Maboresho ya sheria hii yatasaidia ulinzi wa faragha, usalama wa taarifa na uwajibikaji wa taasisi zinazokusanya takwimu ili kuimarisha ubora wake na uaminifu katika takwimu zinazozalishwa.
“Tume imepewa jukumu la kufanya mapitio ya Sheria hiyo ili kupendekeza maboresho kwa serikali.
“Tume ilifanya mapitio haya kwa njia ya utafiti pamoja na majadiliano na wadau mbalimbali, ili kupata maoni yao kwa ajili ya kutoa mapendekezo ya kisheria na ya kiutawala kwa serikali yatakayosaidia kuboresha Sheria husika,””amesema.
Amesema mapendekezo yaliyotolewa yataimarisha mifumo ya kisheria inayohusiana na ulinzi wa data binafsi, ili kuhakikisha kwamba taarifa za wananchi zinafichwa na kulindwa dhidi ya matumizi mabaya.
Amesema sheria hiyo itachangia uwezeshaji wa teknolojia na ubunifu kwa kuweka mazingira bora kwa matumizi ya teknolojia za kisasa katika ukusanyaji na uchambuzi wa takwimu.
Kwa kufanya mapitio hayo amesema sheria hiyo hapa nchini itakuwa na uwezo wa kusaidia maendeleo endelevu na kutoa taarifa sahihi kwa ajili ya uamuzi bora katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kijamii.