Na Yunge Kanuda
WAAJIRI wametakiwa kuwapa wafanyakazi wao haki ya kujiunga na Vyama Vya wafanyakazi kwa ajili ya kuleta tija katika maeneo ya kazi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), Hery Mkunda amesema hayo wakati wa ufunguzi wa semina ya Waajiri na Viongozi wa matawi wa chama hicho Jijini Arusha.
Mkunda amewataka waajiri kufanya hivyo kwa kuwa vyama vya wafanyakazi ni wadau muhimu katika kuchangia maendeleo ya Taasisi.
Amesema tokea mwaka 2018, chama hicho kimekuwa na utaratibu wa kuandaa na kuratibu mafunzo ya pamoja yanayojumuisha washiriki toka Viongozi wa Matawi ya Chama na Mamlaka za Ajira au wawakilishi wao.
“Kwa niaba ya TUGHE niwashukuru sana Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE kwa kukubali kuwezesha na kushiriki mafunzo haya ambapo tayari matunda ya uwepo wa mafunzo haya ya kila mwaka yameanza kuonekana.
“Yameonekana kwa kuwa migogoro baina ya Watumishi na Waajiri imepungua sana na pale ilipojitokeza imekuwa ikipata utatuzi kwa njia ya majadiliano mahala pa kazi,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE Taifa ambaye alikuwa ni mgeni rasmi, Joel Kaminyonge amesisitiza umuhimu wa kuhubiri wajibu na haki sehemu za kazi.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania ( ATE,), Suzanne Ndomba-Doran amesema mada ya haki za msingi za vyama vya wafanyakazi ni elimu muhimu kwa wanachama kwani wanapaswa kufahamu wajibu kwasababu hakuna haki bila wajibu.
Amesema vyama vya wafanyakazi vina wajibu mkubwa wa kuleta utulivu, ufanisi na ukuaji wa tija sehemu za kazi na kuboresha mazingira na mahusiano mazuri baina ya mwajiri na mfanyakazi.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi ( OSHA), amesema nchi inahitaji kuwa na nguvukazi yenye afya njema ili kuleta tija katika maeneo ya kazi hivyo nsuala la Afya na Usalama ni muhimu kuwa agenda endelevu .
Mafunzo hayo ya siku nne yamewakutanisha washiriki kutoka sehemu mbalimbali za kazi zikiwemo Wizara, Idara, Taasisi, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali, Bunge, Mahakama, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Afya za Serikali na zile za binafasi.
Mafunzo hayo yatahitimishwa kwa Washiriki kufanya utalii wa ndani kwa kupata fursa ya kutembelea hifadhi ya Taifa Ngorongoro.