Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limetoa wito kwa Wafanyakazi wote nchini kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kwenda kupiga kura ili kupata Viongozi watakaowaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano ijayo.
Rais wa TUCTA Tumaini Nyamhokya ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha lengo likiwa ni kutoa hamasa pamoja na kuwakumbusha wafanyakazi kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi Mkuu ujao.

Amewataka Wanafanyakazi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kwenda kupiga kura ili tuweze kuwachagua viongozi watakaojali maslahi ya Wafanyakazi.
“Narejea Kauli mbiu yetu ya Mei Mosi 2025, “Uchaguzi Mkuu wa 2025 utuletee viongozi wanaojali haki na maslahi ya maslahi ya Wafanyakazi, Sote Tushiriki’. Sasa ni wakati wa kwenda kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu yetu ili tuhakikishe mika mitano ijayo mambo yetu yanaendelea kuwa safi. Shime sote tushiriki,” amesisitiza .

Katika hatua nyingine Rais wa TUCTA ametumia mkutano huo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na utayari wake kuendelea kutatua changamoto mbalimbali za wafanyakazi na kuzipatia uzito hoja zao zinazowasilisha kwake kisha akataja kwa kifupi machache ambayo amewafanyia wafanyakazi katika kipindi cha uongozi wake.
Katika mkutano huo na wana habari Rais wa TUCTA ameambatana na Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo la
Wafanyakazi Tanzania Hery Mkunda pamoja na Wanachama kutoka Vyama Shiriki vinavyounda TUCTA waliopo katika Jiji la Arusha na mikoa jirani.


