Na Lucy Ngowi
MBEYA: SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limewataka vijana nchini kutambua nafasi yao kama nguvu kazi muhimu kwa maendeleo ya taifa, kuhakikisha wanazitumia fursa zilizopo kwa manufaa yao binafsi na kwa taifa kwa ujumla.
Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA, Rehema Ludanga, amesema hayo katika Kongamano la Siku ya Wafanyakazi Vijana ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Vijana na kuelekea kilele cha Mwenge wa Uhuru Lililofanyika Leo Oktoba 11, 2025 jijini Mbeya.
Amesema vijana wanapaswa kuwa na uelewa mpana kuhusu fursa zinazowazunguka.
“Ni lazima vijana wawe na uwezo wa kutathmini mazingira yao na kutambua fursa mbalimbali ambazo zinaweza kuwa chachu ya maendeleo kwao na kwa taifa. Sisi tunawategemea kuziba mianya ya ajira na nafasi zilizoachwa wazi ili kujenga kesho iliyo bora,” amesema Ludanga.
Ameongeza kuwa moja ya changamoto kubwa zinazolikabili taifa kwa sasa ni mabadiliko ya tabianchi, ambayo yanaathiri sekta muhimu kama kilimo na madini.

Hali hiyo, amesema, inaweza kusababisha kupotea kwa baadhi ya ajira, hivyo vijana wanapaswa kujiandaa kwa kujifunza ujuzi mbadala.
“Katika kipindi hiki cha mpito, ni muhimu vijana kutumia muda wao mwingi kujifunza kazi na ujuzi mbadala zitakazowawezesha kuhimili athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa kongamano hilo lililolenga kuwakutanisha vijana lilikuwa na dhamira ya kuwakumbusha walikotoka, walipo na wanakotaka kuelekea, sambamba na kuweka mikakati ya kujijenga kwa faida yao, familia na taifa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Benno Malisa, amewahimiza vijana kutumia muda wao kwa kujitathmini na kujiuliza serikali inafanya nini kuwawezesha kujitegemea.
“Leo hii mnapigania marupurupu na mishahara kuongezeka. Sawa, lakini mnapoyapata mnapanga vipi matumizi yenu? Je, yanawatosheleza na kuwajenga au yanawabomoa?” amehoji Malisa.

Maadhimisho ya Wiki ya Vijana hufanyika kila mwaka yakilenga kutoa elimu, kuhamasisha ushiriki wa vijana katika maendeleo na kuwajengea uwezo wa kutumia fursa zilizopo kwa manufaa ya taifa.