Na Lucy Ngowi
Katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB) imeelezea fursa zilizopo katika tasnia ya mkonge.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Mkuu wa Sehemu ya Masoko na Uhamasishaji kutoka Bodi ya Mkonge Tanzania, David Magali amesema lengo la ushiriki wao ni kutoa elimu kwa wadau wa mkonge pamoja na kutangaza fursa zilizopo katika mnyororo mzima wa thamani wa mkonge.

“Tuko hapa kuwahamasisha Watanzania kujiingiza kwenye kilimo cha mkonge, uzalishaji wa mbegu, uchakataji wa mkonge pamoja na utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na mkonge.
“Tunaelimisha namna ya kuzalisha mkonge unaokidhi soko la ndani na la kimataifa,” amesema Magali.
Amesema tofauti na mazao mengine, mkonge hauhitaji uangalizi mkubwa, na kwa sasa soko lake ni la uhakika kutokana na mahitaji ya kimataifa kuongezeka.
“Fursa ipo wazi kwa vijana, wanawake na wawekezaji kuingia kwenye kilimo cha mkonge. Ni zao lisilo na changamoto nyingi, lakini lina tija kubwa,” amesema.
Ofisa Kilimo Mwandamizi kutoka Bodi ya Mkonge, Emanuel Lutego amesema ongezeko la wakulima wanaojihusisha na mkonge limechochea hitaji kubwa la mbegu bora.
“Hii ni fursa ya wazi kwa watu binafsi na mashirika kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu za mkonge ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka kila siku,.
“Tunawakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza kwenye mashine za kuchakata mkonge. Lengo letu ni kuongeza uzalishaji wa mkonge hadi kufikia tani 120,000 kwa mwaka, na hilo linawezekana tu tukiongeza uwezo wa uchakataji,” amesema.

Amesema tasnia ya mkonge haimalizii tu kwenye uzalishaji wa nyuzi kwani kuna fursa pana ya kutengeneza bidhaa mbalimbali zitokanazo na mkonge, kama vile mikoba, kamba, mazuria, viatu na hata vipodozi vinavyotumia malighafi ya mkonge.
TSB kupitia vituo vyake vya ubunifu vilivyopo Tanga na Zanzibar, inakaribisha wabunifu na wakufunzi kushiriki katika kutoa mafunzo na kuanzisha viwanda vidogo vya bidhaa zitokanazo na mkonge.
“Hii ni fursa ya kipekee kwa wale wenye mawazo bunifu. Tuna mazingira mazuri ya kuwasaidia kubuni na kutengeneza bidhaa bora kwa soko la ndani na nje,” amesena.
Bodi ya Mkonge inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha elimu ya uzalishaji bora, ufugaji wa mbegu, na uendelezaji wa viwanda inawafikia walengwa kwa ufanisi.