Na Lucy Lyatuu
BODI ya Mkonge Tanzania (TSB) imesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika uchakataji wa mkonge ili kuongeza tija na kufikia lengo la taifa la kuzalisha zaidi ya tani 120,000 kwa mwaka.
Ofisa Udhibiti Ubora Emmanuel Lutego, amesema hayo katika maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama sabasaba yanayoendelea Dar es Salaam.
Amesema Serikali kupitia bajeti yake ya mwaka uliopita imesambaza zaidi ya miche milioni mbili kwa wakulima, na sasa tatizo lililopo ni uhaba wa mashine za kuchakata mkonge,.
Ameongeza kuwa katika mwaka huu wa fedha, serikali inatarajia kusambaza mashine 10 za uchakataji katika maeneo mbalimbali ili kupunguza changamoto hiyo na kuongeza uzalishaji wa mkonge bora, unaokubalika katika soko la dunia.

Mbali na nyuzi, Lutego amebainisha kuwa mabaki ya mkonge hutumika pia kuzalisha bidhaa nyingine zikiwemo mbolea, chakula cha mifugo, uyoga, na nyuzi chuma, hivyo kuongeza thamani ya zao hilo kwa namna nyingi.
Tanzania inatajwa kuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha mkonge bora duniani, na juhudi za Bodi ya Mkonge ni kuhakikisha sifa hiyo inalindwa na kuendelezwa kwa kutumia teknolojia na kuzingatia viwango vya ubora
Mkuu wa Sehemu ya Masoko na Uhamasishaji, David Maghali amesema TSB imetumia Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba kwa kuwataka Watanzania kuchangamkia kilimo Cha mkonge kwani kina tija na soko la uhakika la kimataifa.
Amesema uwepo wao kwenye maonesho hayo ni kwa ajili ya kuwaelimisha wadau kuhusu fursa za kilimo na biashara ya mkonge, pamoja na kuhamasisha ushiriki mpana zaidi wa Watanzania katika sekta hiyo.
Amesema wanatoka elimu juu ya uzalishaji bora wa mkonge ili kuhakikisha kinachozalishwa kinakidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.
“Lengo letu ni kuona wakulima wanazalisha bidhaa zenye ubora ambazo zinanunulika moja kwa moja sokoni,” amesema.
Amesema Tanzania imejaliwa kuwa na ardhi bora kwa kilimo cha mkonge, hivyo ni muhimu kwa wananchi kuitumia fursa hiyo kwa kuwekeza kwenye kilimo hicho ambacho hakina changamoto nyingi na kina soko la uhakika duniani.
“Fursa nyingine ni katika uzalishaji wa mbegu za mkonge, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya miche miongoni mwa wakulima ambayo ni nafasi ya Watanzania kuanza kuzalisha mbegu kwa ajili ya biashara,” amesema.
Aidha, ametaja uanzishaji wa vituo vya uchakataji kuwa ni fursa muhimu, akisema kwa sasa mkonge hauuziwi kama majani bali kwa mfumo wa nyuzi, hivyo ni muhimu kwa wawekezaji kuwekeza kwenye mashine za kuchakata mkonge ili kuongeza thamani ya zao hilo.
Amesema jambo kubwa wanalofanya ni kuhakikisha uzalishaji unalingana na mahitaji ya soko.
“Tuna kituo cha atamizi Tanga kinachotoa mafunzo ya utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na mkonge kama mikoba, mikeka na bidhaa za ufumaji,” amefafanua.
.