Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: CHAMA cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), kinajivunia kwa wafanyakazi wa Reli ya Tanzania na Zambia ( TAZARA), kuweza kupata nyongeza ya mshahara tokea Julai mwaka hu, 2024.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Eddo Makata amesema hayo alipozungumza na Mwandishi wa Mfanyakazi Tanzania kuhusu mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka huu 2024 katika chama hicho.
Amesema, ” Pia upande wa TAZARA tumekuwa na suala zima la kuweza kulilia nyongeza ya mshahara ambayo mfanyakazi wa TAZARA anaipata kwa sababu analipwa kwa dola.

” Kwa hiyo mwezi wa saba mwaka huu wafanyakazi wa TAZARA waliweza kupata nyongeza ambayo iliongeza kima cha chini na kila mfanyakazi aliweza kupata ile nyongeza.
“Kwa hiyo ni jambo tunajivunia kwa sababu tulipigania nyongeza ya mshahara ambayo inatokana na ‘exchange rate’ kwamba mfanyakazi wa TAZARA analipwa kwa dola na katika kulipwa huko kwa dola basi nyongeza yake inapatikana kwa makubaliano yale tuliyokubaliana.
” Na kwamba ikifika asilimia 20 ya dola kupanda basi mfanyakazi huyu tutajadiliana namna ambayo anaweza akapandishwa mshahara wake kwa kutumia hiyo exchange rate,” amesema.
Amesema hayo yamefanyika kwa ushirikiano wa TRAWU na Chama cha Wafanyakazi Zambia.