Na Mwandishi wetu
DODOMA: MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema katika mwaka huu wa fedha 2024/2025 serikali imefanya mabadiliko ya sheria mbalimbali ikiwemo ya kodi itakayoleta unafuu kwa wakulima.
Ofisa Mwandamizi Kodi wa Mamlaka ya Mapato(TRA), Philip Eliamini amesema hayo katika Maonesho ya Wakulima, wafugaji na Uvuvi yajulikanayo kama 88 yanayoendelea Jijini Dodoma.
“Kwa upande wa sheria za kodi kuna misamaha mbalimbali ya kodi ambayo inaenda kuleta unafuu mkubwa kwa wakulima.
“Tunawaomba wakulima waweze kutembelea banda la TRA wapate elimu ya misamaha ya kodi ambayo imepitishwa na bunge ili waweze kupata elimu hiyo na kujua zana ambazo zimesamehewa kodi,” amesema.
Amesema mabadiliko ya sheria ya mwaka jana yaliweka kipengele cha kila raia kuanzia miaka 18 na kuendelea anapaswa kuwa na namba ya utambulisho wa mlipa kodi.
Amesema TRA inatoa namba ya utambulisho wa mlipa kodi, kikubwa mtu awe na namba ya NIDA.
Vile vile wanatoa huduma ya makadirio ya kodi kwa mfanyabiashara ambaye bado hajakadiriwa makadirio ya kodi kwa mwaka huu wa fedha
Kwa upande mwingine amesema maonesho hayo yanatoa fursa kwa TRA ya kuonana na wananchi kwa ajili ya kuwapa elimu ya kikodi, usimamizi wa kodi lakini pia kupokea maoni na malalamiko ya wananchi yanayowawwzesha kuboresha utendaji wao wa kila siku.
“Kwa hiyo tunasema maonesho haya ni fursa nzuri kwa wananchi kujifunza lakini pia ni fursa nzuri kwetu ambapo tunaweza kuonana na wadau wetu na tunawapa elimu ambayo itawasaidia katika shughuli zao.”amesema.