Na Lucy Ngowi
DODOMA: MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA), inatoa elimu ya namna sahihi ya kutumia viuatilifu katika mashamba ya wakulima ili kuweza kudhibiti visumbufu vya mazao.
Aidha mamlaka hiyo inatoa maelekezo ya jinsi ya kujisajili kwa wale wanaotaka kuingia kwenye biashara ya viuatilifu.
Ofisa Mwandamizi wa Udhibiti wa Visumbufu kwa Njia ya Kemikali kutoka Kitengo cha Usimamizi wa Matumizi sahihi ya Visumbufu, Edmund Luena amesema hayo katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea jijini Dodoma.
Luena amesema upande wa elimu ya matumizi sahihi ya viuatilifu hufundisha wakulima namna gani sahihi ya kufanya.
“Tunaposema matumizi sahihi ya viuatilifu huwa tunaanzia na utambuzi wa kiumbe anayeharibu mazao yakiwa shambani kwa mfano wadudu waharibifu, ndege, vimelea vya magonjwa, magugu au panya,”amesema.
Amesema katika maonesho hayo wapo kuelezea namna gani mkulima achukue hatua ili kudhibiti visumbufu.
“Tuna teknolojia ya kutumia njia tofauti na kemikali japo mamlaka inahusika na udhibiti wa biashara ya viuatilifu lakini pia tunatoa elimu ya njia nyingine tofauti na kemikali kama njia za kibaolojia na utumiaji wa mitego,” amesema
Amesema kwa njia ya kutumia kemikali wanayo mabomba wanaelekeza wakulima namna gani wanaweza kutumia hayo mabomba kwa usahihi.
Amesema kosa likifanyika kwenye kile kifaa kinachotoa matone, kiuatilifu hakifanyi kazi kwa usahihi.
Amesema na bomba kama halitosis vizuri ile sumu , wanaelekeza namna gani ili lile bomba litoe mnyunyizo inavyotakiwa.