Na Lucy Ngowi
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru ameelezea vipaumbele vya mamlaka hiyo kuwa ni kuwajengea uwezo wataalamu katika kusimamia udhibiti wavisumbufu.
Profesa Ndunguru ametaja vipaumbele hivyo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Mimea Mei 12, mwaka huu 2025 katika Viwanja vya Makumbusho ya Azimio La Arusha mkoani Arusha.
Pia ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuweka mifumo ya ufuatiliaji wa viashiria vya uwepo wa milipuko ya visumbufu.
Kuendelea kusimamia matumizi sahihi ya viuatilifu, pamoja na kuanzisha mfumo wa kufuatilia masalia ya viautilifu kwenye mazao yauzwayo kwenye masoko ya ndani.
Vile vile kuimarisha miundombinu ya ukaguzi mipakani kwa kuanzisha maabara ndogo kwenye mipaka 17, kufungua ofisi na maabara mkoa wa Njombe kwa ajili ya kuhudumia mazao ya kimkakati, hususan parachichi, viazi mviringo na mboga mboga.
Profesa amesema ikiwa ni pamoja na kuendelea kumarisha udhibiti wa visumbufu kwa njia ya kibailojia – viuatilifu hai, viumbe rafiki.