Na Lucy Ngowi
MAMLAKA ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), ina mchango mkubwa katika utoshelevu wa chakula kwa asilimia 128 kwa kudhibiti visumbufu vya mazao ambavyo vingeweza kuathiri uzalishaji wa mazao hayo.
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya ya Mimea Mei 12, mwaka huu 2025 katika Viwanja vya Makumbusho ya Azimio La Arusha mkoani Arusha.
Ametolea mfano wa jinsi mamlaka hiyo ilivyofanikiwa kudhibiti baa la panya katika mikoa 16, wilaya 54, kata 540 na kuokoa jumla ya ekari 358,895 za mazao ikiwemo mahindi.
“Hadi kufikia Aprili 2025 TPHPA imefanya udhibiti wa ndege aina ya kwelea kwelea milioni 200.7 katika hekta 220,163 za halmashauri 18 na kuokoa zaidi ya tani 1,463,445, ikiwemo mpunga, uwele na mtama.
“Kudhibiti viwavi jeshi katika hekta 83,180 na kuokoa zaidi ya tani 332,732 za mazao ya nafaka ikiwemo mahindi katika mashamba mbalimbali.
“Kudhibiti Nzige ekari 1340 waliovamia wilaya ya Mpwapwa mkoa wa Dodoma, pamoja na nzige wekundu milioni 36 waliovamia ekari 405 wilaya ya Ikungi Mkoa wa Singida,” amesema.
Pia amesema mamlaka hiyo imewezesha ufunguaji wa Masoko Mapya ya mazao ya kilimo Nje Ya Nchi.
“Mamlaka imewezesha ufikiaji wa masoko kwa mazao tisa ya kipaumbele katika nchi 14. Kati ya Mazao tisa yaliyohusika katika ufunguzi wa masoko Kimataifa, na Nchi husika yanakosafirishwa,” amesema.
Ametaja mazao hayo kuwa ni Vanilla yanasafirishwa China, Indonesia na India. Parachichi yanasafirishwa Canada, Malaysia, Afrika Kusini, India, China na Umoja wa Ulaya, Israel.
Pia ndizi zinasafirishwa Afrika Kusini, Viazi mviringo nchini Zambia,Kahawa na soya nchini China, Nanasi China, India, uturuki na Brazil.
Vile vile Karafuu Indonesia na Singapore, Pilipili Manga nchini Canada, Kakao nchini Marekani, Tumbaku nchini Iraki na Pakistan.
Pia TPHPA imefanikiwa kufungua masoko mapya ya parachichi nchini Afrika Kusini, India na China, Soya nchini China, Mashudu, Pamba na Alizeti nchini China na mahindi ya njano nchini Misri.
Amesema biashara hiyo ya mazao ikifanyika itaingizia Tanzania kiasi cha dola za kimarekani bilioni 3.5 kwa mwaka.