Yatoa Elimu kwa Maelfu Nane Nane
Na Lucy Ngowi
DODOMA: MBEGU bora inalipa! Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI), Nyasebwa Chimagu ametoa ujumbe huo leo Agosti nane, 2025
katika maonyesho ya wakulima ya Nane Nane yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma.
Chimagu amesema katika maonyesho hayo, TOSCI imeeleza kwa kina namna mbegu bora si tu nyenzo ya kuongeza tija katika kilimo, bali pia ni chanzo muhimu cha ajira na biashara.
Amesema mtu anaweza kujiajiri kwa kuzalisha mbegu, kuuza, kuwa wakala au kuajiriwa viwandani kwenye uchakataji wa mbegu.
“Tumetoa elimu ya kutosha kwa wananchi na hadi kufikia jana, Agosti Saba, 2025 watu 3,618 walifika kwenye banda letu, wengi wao wakijiandikisha kama wafanyabiashara wanaotaka kusajiliwa ili wawe sehemu ya mnyororo wa usambazaji wa mbegu bora.
“Hili ni moja ya mafanikio makubwa ya ushiriki wetu kwenye maonyesho haya,” amesema Chimagu.
Amesema taasisi hiyo ya serikali ina dhamana ya kudhibiti na kuhakikisha ubora wa mbegu kuanzia hatua ya uzalishaji mashambani hadi zinapofika sokoni.
Pia amesema taasisi hiyo imeshathibitishwa kimataifa, hivyo mbegu zinazokaguliwa na kuthibitishwa na TOSCI zinaweza kuuzwa ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia viwango vya ubora wa kimataifa.
Amesema Katika banda la taasisi hiyo, wamewaelimisha wakulima jinsi ya kujiridhisha na ubora wa mbegu kwa kutumia mfumo wa kidijitali:
Kupitia simu kwa kupiga *148*52#, mkulima anaweza kuingiza namba ya vocha iliyopo kwenye mfuko wa mbegu na kujua kama mbegu hiyo ni halali au feki.
“Tumepokea malalamiko ya mbegu feki sokoni na tayari baadhi ya wauzaji wamekamatwa. Tunaendelea kutoa elimu kwa wakulima ili wasinunue mbegu bila uthibitisho wa ubora,” amesema.
Amesema Katika kusukuma mbele ajenda ya kulisha dunia, Rais Samia Suluhu Hassan kupitia msimu wa kilimo 2024/2025 alianzisha mpango wa ruzuku ya mbegu bora za mahindi, zao linalochangia zaidi ya asilimia 60 ya mazao ya nafaka nchini.
Amesema Katika maonyesho hayo, taasisi hiyo imetumia jukwaa hilo kuhamasisha usajili wa wakulima kwenye mfumo wa kidijitali ili waweze kunufaika na ruzuku hiyo.
Hivyo hadi kufikia jana Agosti saba, 2025, wakulima 5,156 walikuwa wamesajiliwa kupitia maonyesho ya Nane Nane pekee.
“Tumeona fursa hii imefika kwa wakulima waliokosa elimu au njia ya kusajiliwa kwenye maeneo yao. Sasa wanaweza kununua mbegu bora kwa bei nafuu kupitia ruzuku,” amesema.
Amesema Maonyesho ya kitaifa ya wakulima ya Nane Nane ambayo hufanyika kila mwaka yamekuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya kilimo.
Mwaka huu yalifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango huku yakiwa na kaulimbiu isemayo:
‘Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi’.
TOSC imetumia maonyesho haya si tu kuonyesha mafanikio ya taasisi hiyo, bali pia kuelimisha jamii juu ya nafasi ya mbegu bora katika maendeleo ya kilimo, biashara, na ajira.
Mkurugenzi Chimagu ametoa wito kwa wakulima wote nchini ambao hawajasajiliwa, watembelee ofisi za kilimo za kata au vijiji ili wapate nafasi ya kusajiliwa na kunufaika na ruzuku ya mbegu kabla msimu wa kilimo haujaanza.
“Huu ndio wakati sahihi wakulima wanapokuwa na fedha baada ya kuuza mazao yao. Tuwahimize wanunue mbegu bora, kwa sababu mbegu bora ndiyo msingi wa mavuno bora,” amesema.