Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imeweka mikakati thabiti ya kutekeleza miradi ya ujenzi na uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia kwa vitendo katika shule na vyuo vya mafunzo ya amali nchini.
Mikakati inayolenga kuboresha elimu ya amali na kuwawezesha vijana kujiajiri.

Mwenyekiti wa Bodi TEA, Dkt. Leonard Akwilapo amesema hayo katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yajulikanayo kama Saba Saba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam.
Amesema Mamlaka hiyo imepewa fedha za kutosha ili kutekeleza miradi hiyo muhimu katika shule teule zinazotoa mafunzo ya amali.
“Tumepewa fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi katika shule teule zinazotoa mafunzo ya amali,” amesema Dkt. Akwilapo.

Pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuiwezesha TEA kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao umekuwa kichocheo kikuu cha mageuzi katika sekta ya elimu nchini, hususan katika kukuza ujuzi na uwezo wa kujitegemea kwa vijana.
Mamlaka hiyo inatekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu ya amali kama vile karakana, madarasa ya vitendo, mabweni na vifaa vya kisasa vya kujifunzia, sambamba na kutoa ufadhili wa mafunzo kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF).
Hadi sasa, maelfu ya vijana wamenufaika na mafunzo hayo na wameweza kujiajiri katika sekta mbalimbali ikiwemo useremala, umeme, uashi, ushonaji na ICT.
Katika maonyesho hayo ya kimataifa, TEA inalenga kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kupanua wigo wa huduma zake na kusambaza elimu kwa umma kuhusu mipango ya kukuza elimu ya amali nchini.

Kupitia ushiriki wake katika Maonyesho ya Saba Saba, TEA inasisitiza dhamira yake ya kuandaa mazingira bora ya elimu ya vitendo ili kuhakikisha Tanzania inazalisha nguvu kazi yenye ujuzi wa kutosha kwa ajili ya maendeleo ya taifa.