Na Mwandishi Wetu
DODOMA: MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA), ina jukumu kubwa la kuhakikisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia yanaboreshwa kwa viwango vinavyohitajika.
Kutokana na jukumu hilo, imejipanga kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia mafunzo ya amali kama sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Mkurugenzi Mkuu TEA, Dkt. Erasmus Kipesha amesema hayo wakati wa maonesho ya uzinduzi wa Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 Toleo la 2023, Jijini Dodoma.
“Jukumu la TEA ni kusimamia uboreshaji wa miundombinu ya kujifunzia na kufundishia,” amesema.

Amesema utekelezaji wa sera mpya ya elimu unahitaji miundombinu imara na vifaa vya kutosha kwa ajili ya mafunzo ya amali.
Dkt. Kipesha ameeleza kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haiwezi kutekelezwa kwa ufanisi bila kuboresha miundombinu.

Amesema kwa mwaka huu wa fedha, Shilingi takribani Bilioni tatu zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na uboreshaji wa miundombinu katika shule 20, zinazotoa mafunzo ya amali.
Amesema mafunzo hayo ya amali ni latika fani za kilimo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), mapishi, ushonaji, michezo na sanaa.

Katika kutekeleza Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, TEA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu kutafuta rasilimali fedha ili kuhakikisha miundombinu ya mafunzo ya amali inaboreshwa na vifaa vinapatikana kote nchini.