Na Lucy Ngowi
GEITA: WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), imetenga Sh milioni 580 kukamilisha barabara za kilomita 210, hasa zinazohusiana na shughuli za madini.
Meneja wa TARURA mkoa wa Geita, David Msechu amesema hayo alipozungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya nane ya sekta ya madini yanayoendelea mkoani Geita
Amesema fedha hizo zimetengwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 hadi 2025/2026, na kwamba hadi sasa baadhi ya kazi zimekamilika huku nyingine zikiendelea kutekelezwa.

Amesema TARURA wapo katika maonesho hayo ili kutoa elimu kwa umma kuhusu kazi wanazofanya katika kusimamia mtandao wa barabara za wilaya nchini.
Amesema taasisi hiyo inasimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara zenye jumla ya kilomita 100,044 nchi nzima, ambapo Geita pekee ina kilomita 7,264 na asilimia 60 ya mtandao huo unapitika. Kati ya hizo, kilomita 564 zinahudumia maeneo ya shughuli za madini.
Pia amesema TARURA inajivunia maabara ya kisasa inayopima ubora wa barabara na kazi nyingine za ujenzi.
Kwamba, maabara ya Geita imesaidia miradi mbalimbali kama ule wa umwagiliaji Ibanda, kituo cha umeme Nakayazi (TANESCO), na miradi ya
Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), na Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu kwa Ajili ya Ustawi wa Jamii na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi (TACIP).

Aidha, TARURA Geita inatekeleza ujenzi wa madaraja kwa kutumia teknolojia ya mawe, ambapo tayari madaraja manne yamekamilika. Teknolojia hiyo inalenga kuongeza ubora na kupunguza gharama.
Amesema changamoto kubwa inayokabili barabara za maeneo ya madini ni magari makubwa kupita kwenye barabara zisizokidhi uzito zaidi ya tani 10.
Hivyo amesema wakala huo unatoa wito kwa wananchi na wawekezaji kushirikiana ili kuhakikisha barabara hizo zinaboreshwa kwa manufaa ya wote.

Kwa upande wake, Mhandisi Faiza Mbange kutoka makao makuu ya TARURA amesema wapo kwenye maonesho kutoa elimu kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya barabara, kulinda miundombinu, na kutoa ufafanuzi kuhusu masuala ya fidia kwa maeneo ya miradi.
Kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia, TARURA inatarajia kujenga kilomita 59 za barabara katika wilaya ya Mbongwe mkoani Geita, ambapo usanifu wa barabara tatu tayari umekamilika na hatua ya kumpata mkandarasi inaendelea.