Na Lucy Ngowi
DODOMA: UJENZI wa madaraja ya mawe 275 nchini, ndani ya miaka saba umetumia takribani sh bilioni 10 , kiasi hicho cha fedha kikiwa ni kidogo, tofauti kama yangejengwa ya zege.
Mhandisi Mshauri kutoka Wakala wa Barabara ya Vijijini na Mijini ( Tarura), Phares Ngeleja ameeleza hayo katika Maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi yanayoendelea Nzuguni jijini Dodoma.
Ngeleja amesema, ” Kwa mfano tunajenga madaraja ya mawe ambayo gharama yake ni nafuu zaidi ukilinganisha na daraja la zege,”.

Amesema gharama ingekuwa kubwa na kufikia sh bilioni 50, kama wangejenga madaraja hayo kwa kutumia nondo na zege.
“Kwa hiyo utaona utofauti mkubwa ambao tumeweza kuokoa hela nyingi sana ambazo zingeweza kutumika kwenye kazi nyingine.
Amesema njia hiyo ya kutumia mawe ni nafuu, hivyo TARURA imeona ili waweze kuifungua nchi kwa kipindi lifuoi hakuna budi kutumia teknolojia zinazotumia gharama nafuu.
Akizungumzia barabara amesema wanajenga kwa kutumia teknolojia mbalimbali ikiwemo ya mawe ambayo wameitumia mikoa ya Mwanza,Kigoma. Rukwa na Morogoro.
Amesema kwenye barabara wanashirikiana na wadau mbalimbali katika ujenzi wa gharama nafuu.