Na Lucy Ngowi
MOROGORO: WAKULIMA pamoja na wadau wa kilimo nchini wamealikwa kutembelea Maonesho ya Wakulima yajulikanayo kama Nanenane ili kupata maarifa na teknolojia bora za kilimo.
Akizungumza katika Maonesho ya Kanda ya Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Ilonga kilichopo Kilosa mkoani Morogoro, Dkt. Arnold Mushongi amesema maonesho hayo ni fursa muhimu kwa wakulima kupata ujuzi wa kisasa.
Amesema mbali na maonesho ya Nanenane, TARI imeweka wataalam wawili pamoja na watumishi watatu watakaokuwepo kwa muda wa mwaka mzima ili kutoa huduma kwa wakulima.
Katika eneo hilo la maonesho, TARI imepanda mazao yote yanayostawi vizuri katika Kanda ya Mashariki na maeneo mengine ya nchi.

“Kuna teknolojia ya mbegu bora, teknolojia za agronomia, teknolojia za udhibiti wa visumbufu, pamoja na teknolojia za kilimo biashara, masoko, baada ya mavuno na kuongeza thamani ya mazao kupitia usindikaji,” amesema.
Dkt. Mushongi ameongeza kuwa shughuli hizo haziendeshwi na TARI peke yake, bali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoka kwenye miradi ya wafadhili na vikundi vya wakulima.

“Vipando vya mazao ya nafaka, mikunde, mizizi, mazao ya kibiashara kama miwa na mkonge, pamoja na kilimo misitu, migomba na pamba vyote vimepandwa ili kumwonyesha mkulima na mdau wa mnyororo wa thamani,” amesema.
Pia amesema katika uwanja huo TARI imeweka miundombinu ya umwagiliaji maji wakati wote wa mwaka, “Itachangia kuwa Hub ya uhaulishaji teknolojia na mafunzo muda wote wa mwaka,”.

Amesisitiza kuwa TARI imepewa jukumu kubwa la kufanya, kusimamia, kuratibu na kuendesha tafiti mbalimbali zinazolenga kuboresha kilimo nchini.
Kanda ya Mashariki inahusisha mikoa minne ambayo ni Morogoro, Pwani, Dar es Salaam na Tanga.