Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: KATIKA Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yajulikanayo kama Sabasaba, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imeonyesha jinsi teknolojia na uvumbuzi vinaweza kubadilisha maisha ya wakulima na kuchochea maendeleo ya kilimo kwa ujumla.

Akizungumza na Mfanyakazi Tanzania katika banda la TARI, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt. Thomas Bwana amesema maonyesho hayo ni jukwaa muhimu la kukutana na wadau mbalimbali, hasa wakulima, wajasiriamali, na wafanyabiashara, kwa ajili ya kuonesha teknolojia mpya zinazotatua changamoto za sekta ya kilimo.
“Wajibu wetu mkubwa ni kuhakikisha tunaibua na kuendeleza teknolojia zitakazosaidia wakulima kuongeza tija, kupunguza gharama na kuongeza kipato,” amesema.
Amesema miongoni mwa uvumbuzi uliovutia wananchi ni mashine ya ‘Rafiki Planter’, inayotumika kupanda mbegu za pamba kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.
“Kwa kawaida, hekta moja ya pamba hupandwa na watu 10 hadi 16 ndani ya saa nane, lakini kwa mashine hiyo, kazi hiyo hufanyika kwa saa moja tu na mtu mmoja.
“Hii inamaanisha wakulima wanaweza kuwahi mvua, kupunguza gharama za kazi na kuongeza uzalishaji,” amesema.
Amesema kupitia tafiti za TARI, nafasi za upandaji wa pamba zimeboreshwa kutoka sentimita 90×40 hadi 60×30. Mabadiliko haya yameongeza idadi ya mimea kutoka 22,000 hadi zaidi ya 44,000 kwa hekta moja, na kuongeza mavuno kutoka kilo 1,200 hadi kati ya kilo 2,400 na 2,700 kwa hekta.
“Tija imeongezeka, na mara moja fedha zimeanza kuingia mfukoni mwa mkulima,” amesema.

Amesema taasisi hiyo pia ipo na mbegu bora za migomba zinazozalisha mikungu yenye hadi kilo 94, ikilinganishwa na wastani wa kilo 30 za migomba ya kawaida. Kwa upande wa mihogo, mbegu aina ya TARICASS 4 imeongeza uzalishaji karibu mara tano zaidi ya mihogo ya kawaida.
Amesena Katika eneo la kuongeza thamani, TARI imeonyesha matumizi mbadala ya mihogo, mtama, uwele na korosho.
“Mihogo sasa inaweza kutumika kutengeneza tambi, biskuti, mikate, na hata unga wa biashara badala ya kutegemea ngano pekee.
“Kwa korosho na karanga, taasisi imeonyesha teknolojia za kuongeza thamani kwa kutengeneza siagi, unga wa korosho, na bidhaa zilizoimarishwa kwa virutubisho.
“Mabibo ya korosho ambayo hapo awali yalionekana kuwa taka, sasa hutumika kutengeneza juisi, divai na hata ethanol kwa ajili ya vitakasa mikono,” amesema.
Amesema katika mazao ya nafaka kama mtama na ulezi, TARI imefanikiwa kutengeneza bidhaa kama maandazi, hatua inayochochea wajasiriamali kuibua bidhaa mpya sokoni huku wakulima wakinufaika kwa kuuza mazao yenye thamani zaidi.
Ametoa wito kwa wajasiriamali na wakulima kutembelea taasisi hiyo na kujifunza teknolojia mbalimbali zinazoweza kuwapatia fursa za biashara na kukuza kipato.
“Lengo letu ni kuhakikisha matokeo ya utafiti hayabaki makaratasi; tunataka yawe suluhisho la maisha ya Watanzania,” amesema.