Na Mwandishi Wetu
TANZANIA inashiriki katika Kongamano la Afya la Dunia linalofanyika kwa siku tatu jijini Berlin, Ujerumani lililoanza Oktoba 12 hadi 14, mwaka huu 2025.
Aidha ujumbe kutoka Tanzania umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ismail Rumatila.

Taarifa imesema Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Hassani Mwamweta, naye ameshiriki kongamano hilo linalofanyika lenye kaulimbiu ‘Kuchukua Jukumu la Afya katika Ulimwengu unaogawanyika’.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Kongamano hilo limekusanya watu wa kada mbalimbali duniani wakiwemo viongozi wa serikali, taasisi za kimataifa, asasi za kiraia, sekta binafsi, wataalam wa afya, watafiti, wanasayansi, na wanaharakati kujadili namna ya kupata ufumbuzi wa changamoto za kiafya zinazoikabili dunia.

Imesema katika siku ya ufunguzi Washiriki walijadili mada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuimarisha ushirikiano baina ya nchi katika sekta ya afya, pamoja na umuhimu wa kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza,
Yakiwemo kisukari, moyo, figo, na kansa ambayo yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa idadi ya vifo duniani.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika, Profesa Mohamed Janabi, alikuwa mmoja wa wachangia mada hizo zilizokuwa zikiendeshwa kwa utaratibu wa paneli.
Serikali imekuwa ikishiriki majukwaa kama hayo kwa lengo sio tu la kupata wadau wa kushirikiana nao kuimarisha sekta ya afya nchini, bali pia kujiimarisha kidiplomasia katika anga za kimataifa.
