Na Lucy Lyatuu, Dodoma
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema ushiriki wa Wanawake na Wasichana katika sayansi ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kiuchumi.
Amesema Tanzania inalenga kufikia angalau asilimia 51 ya ushiriki wa wanawake katika sayansi na kwamba Serikali inaendelea kuwekeza ili kuongeza wataalam katika nyanja hiyo.
Profesa Mkenda ametoa kauli hiyo jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Siku ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi, akieleza kuwa sayansi ni msingi wa maendeleo kwani huongeza tija katika uzalishaji na kutoa suluhisho la changamoto mbalimbali kijamii kupitia tafiti na matumizi ya teknolojia.
Amesema takwimu zinaonesha takribani wanawake asilimia 36 Duniani, ni wataalamu wa sayansi na kwamba Tanzania inalenga kufikia angalau asilimia 51 ya ushiriki wa wanawake..
Aidha, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuongeza fursa za elimu, ikiwemo ufadhili wa masomo kupitia Samia Skolashipu, kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kusoma fani za Sayansi, TEHAMA, Uhandisi na Sayansi Asilia.
Maadhimisho ya Wanawake na Wasichana katika Sayansi kwa mwaka 2026 yamekwenda sanjari na uzinduzi wa Kampeni ya “Africa Educate Her” nchini Tanzania, inayolenga kuongeza upatikanaji wa elimu kwa wasichana na kuwapa fursa sawa za kujifunza na kufanikiwa.


