Na Lucy Ngowi
LUSAKA – ZAMBIA: TANZANIA imeibuka mshindi wa pili kati ya nchi 25 zilizoshiriki Maonesho ya 97 ya Kimataifa ya Kilimo na Biashara yaliyofanyika Lusaka, Zambia, kuanzia Julai 29 hadi Agosti nne, mwaka huu 2025, Zimbabwe ikishika nafasi ya kwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti nane, 2025 katika ukumbi wa MOI, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema ushindi huo umetokana na elimu na maelezo ya kitaalamu kuhusu huduma za afya za kibingwa na kibobezi kutoka Tanzania, pamoja na mchango wa sekta ya usafirishaji.

“Taasisi tano kutoka Tanzania zilishiriki, zikiwemo MOI, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya (MZRH), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), na Shirika la Ndege la ATCL. Kwa pamoja tumefanya vizuri na kushika nafasi ya pili,” amesema.
Amesema ushiriki wa taasisi za afya ulilenga kuhamasisha utalii wa tiba, kwa lengo la kuwavutia wagonjwa kutoka Zambia kuja kupata huduma bora za afya Tanzania badala ya kwenda nje ya bara la Afrika ambako gharama ni kubwa.
“MOI na JKCI tunatoa zaidi ya asilimia 96 ya matibabu ya magonjwa ya moyo, mifupa, ubongo na mishipa ya fahamu. Tukiwa Zambia, taasisi hizi tatu za afya ziliweza kuhudumia watu 911, kati yao 105 wameahidi kuja Tanzania kwa matibabu zaidi,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii Tiba Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema kamati hiyo imewekeza nguvu kubwa katika kujitangaza ili kuwavutia wagonjwa kutoka mataifa mengine kuja kutibiwa Tanzania.
“Awali tulikwenda visiwa vya Comoro na kutoa huduma kwa watu 2,292. Hadi sasa tumepokea wagonjwa zaidi ya 150 waliokuja kutibiwa katika hospitali zetu za MOI, MNH, JKCI na Ocean Road. Haya ni matunda ya ushiriki wetu kwenye maonesho kama haya,” amesema Dkt. Kisenge.
Amesema kuja kwa wagonjwa kutoka nje kunachangia ukuaji wa uchumi wa taifa:, “Watakuja kulala katika hoteli, kununua chakula na kupata huduma mbalimbali, haya yote yanaongeza pato la taifa. Ndiyo maana tunaita tiba utalii mtu anatembelea nchi yetu kwa ajili ya kupata matibabu.”
Ushiriki wa Tanzania uliratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Zambia chini ya Balozi Mathew Mkingule. Banda la Tanzania lilitembelewa pia na Rais wa Zambia, Hakainde Hichelema, Agosti mbili, 2025.