Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM: TANZANIA imeweka malengo makubwa ya kupanua ushirikiano wake wa kiuchumi na Uturuki kwa kufikia biashara ya thamani ya Dola za Kimarekani Bilioni moja, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi kupitia diplomasia ya biashara.
Akizungumza Mkoani Dar es Salaam wakati wa kusainiwa kwa Azimio la Kamati ya Pamoja ya Biashara (JTC) kati ya Tanzania na Uturuki, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, amesema hatua hiyo inalenga kuongeza thamani ya bidhaa za Tanzania zinazopelekwa kwenye soko la Uturuki.

“Kupitia timu ya wataalamu na ushirikiano wa sekta binafsi, tutaweka msingi imara wa kukuza mauzo yetu na kuifanya biashara kuwa lango kuu la fursa kwa wananchi wetu,” amesema Dkt. Jafo.
Dkt. Jafo amesema kuna fursa kubwa ambazo bado hazijatumika kikamilifu katika sekta za viwanda, kilimo, na madini, huku akisisitiza kuwa Tanzania inajifunza teknolojia ya kisasa kutoka kwa washirika wao wa Uturuki ili kuongeza ufanisi wa uzalishaji wa ndani.
“Teknolojia ya Uturuki kwenye viwanda na kilimo ni ya kiwango cha juu. Ushirikiano huu utatufungulia milango ya maarifa na kuongeza tija kwa Watanzania,” amesema.
Uhusiano kati ya Tanzania na Uturuki umeimarika kwa kasi katika muongo uliopita, hasa kufuatia kufunguliwa kwa balozi za nchi hizo mwaka 2009 na 2017 mtawalia. Ziara za viongozi wakuu — akiwemo Rais Recep Tayyip Erdoğan na Rais Samia Suluhu Hassan — zimechochea zaidi mashirikiano hayo.
Kwa upande wake, Kaimu Balozi wa Uturuki nchini Tanzania, Ali Goktug IPEK, amesema kuwa JTC itakuwa chombo muhimu cha kuondoa vikwazo vya kibiashara na kurahisisha uwekezaji kati ya pande hizo mbili.
“Tutaendelea kushirikiana kwa karibu katika maeneo ya miundombinu, kilimo, nishati na teknolojia. Kamati hii itakuwa jukwaa la maendeleo ya pamoja,” amesema IPEK.
Amehitimisha kwa kusema kuwa chini ya uongozi wa Rais Erdoğan na Rais Samia, nchi hizo mbili zitajenga uhusiano wa kiuchumi wenye misingi ya uadilifu, maendeleo na ustawi wa pamoja.