Na Danson Kaijage.
TANZANIA itakuwa mwenyeji wa kongamano la Kimataifa la eLearning Africa linalotarajiwa kufanyika Mei saba hadi tisa, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa.Adolf Mkenda amesema hayo alipozungumza na Waandishi wa Habari kuhusu ujio wa kongamano hilo.
Amesema kongamano hilo hapa nchini litakuwa la mara ya pili kufanyika.

Profesa Mkenda amesema lengo la kongamano hilo ni kuleta kwa pamoja makundi mbalimbali kutoka zaidi ya nchi 65 kwa ajili ya kujadili, kubadilishana uzoefu, kuhamasisha uwekezaji na kuazimia mipango ya pamoja ya kuchagiza matumizi ya Teknolojia za kidijitali katika Sekta ya Elimu Barani Afrika.
Amesema kongamano kama hilo lishafanyika nchi 17 ikiwemo Tanzania.
“Kongamano hilo Tanzania lilifanyika mwaka 2021 hivyo mwaka huu litakuwa linafanyika kwa mara ya pili, litawakutanisha wadau mbalimbali Barani Afrika.,” amesema.

Amesema makundi hayo ya wadau yatajumuisha watunga sera,watoa maamuzi,wataalamu wa Elimu,wataalamu wa Teknolojia,watafiti,wabunifu,wafanya biashara,wawekezaji na wadau wa maendeleo.
Pia kongamano hilo litajumuisha mkutano wa mawaziri zaidi ya 50 kutoka nchi 49 Barani Afrika utakao kuwa na lengo la kuazimia mikakati ya pamoja na kuandaa nguvu kazi maili katika kubuni, kuzalisha,na kuimalisha matumizi ya kidigitali.
“Kama wenyeji wa kongamano hili nchi yetu inatarajia kunufaika na fursa mbalimbali kutokana na kuwa mwenyeji wa kongamano hili ambapo tutabaini mikakati mpya hususani katika sekta ya Elimu,” amesema.
Kauli mbiu ya kongamano inasema ‘Kufikiria Upya Elimu na Maendeleo ya Raslimali Watu kwa Ustawi wa Afrika’.