NA Lucy Lyatuu
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco), limewahakikishia watanzania kuendelea kuwapatia elimu juu ya matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia.
Mkurugenzi Mtendaji
Lazaro Twange amesema katika kutoa elimu hiyo Tanesco imetoa zawadi ya majiko ya umeme kwa Wananchi waliofika katika banda lao lililopo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama sabasaba.
Akizungumza na waandishi wa katika viwanja vya maonesho hayo, Mkurugenzi Twange amesema wananchi waliofika katika banda lao wamepata fursa ya kupata elimu ya nishati safi ya kupikia na kupatiwa majiko.

“Ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwamba watanzania tuhame kwenye kutumia nishati isiyokuwa safi na kutumia iliyosafi, hivyo hapa tunazungumzia nishati ya umeme na tuna majiko haya ya umeme yamefanyiwa utafiti na kuthibitika kuwa unaweza kupikia na chakula kikaiva kwa kutumia chini ya Unit moja tu.
“Kupitia maonesho haya tumeona ni vema wananchi tuwapatie maswali na wale wanaojibu vema maswali waliyoulizwa wamepata fursa ya kujishindia zawadi ya majiko hayo ya kupikia”amesisitiza
Aidha amewashukuru watanzania waliofika katika banda lao na kuwapatia elimu kuhusu masuala ya nishati safi yakupikia.
Naye Kaimu Meneja Mkuu wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), Sadock Mugendi amesema wamekuwa wakisambaza na kusafirisha umeme maeneo mbalimbali vijijini na kwamba hivi karibuni wamemaliza mradi wa kusafirisha umeme kutoka Tabora mjini kuelekea Katavi wenye kilomita 383 na una msongo wa Kilovolt 132.”