Na Lucy Ngowi
DAR ES SALAAM: TAASISI ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), inapambana kuzuia mabadiliko ya Tabianchi kwa kufanya tafiti zinazowezesha wananchi kutumia nishati mbadala badala ya kuni.
Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dkt.Ismael Kimirei amesema hayo wakati akichangia mada katika Kongamano la tisa la Sayansi, Teknolojia na Ubunifu pamoja na maonesho lililoandaliwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) lililomalizika hivi karibuni.
Kimerei amesema,”Tumeanza na Tanga kutumia sola lakini sola hiyo sio ya kawaida kuweka samaki juani kama hao mwanzo, sasa hivi tunajenga mabanda ambayo bado tunaweza tukatunza lile kusudi hata kama hakuna jua la kutosha bado mtu anaweza akakausha samaki.
“Kwa hiyo kwa style hiyo tunakuwa tumepunguza kutengeneza kwenye kuni katika kukausha samaki,” amesema.
Vilevile amesema,”Kule Tanganyika tumetengeneza jiko banifu. Kwa mfano ulitumia kilo 100 za kukausha kilo 100 za dagaa, nitumie kilo 20 au kilo mbili za kuni kukausha kilo ile ile 100. Unaangalia utafiti wetu unajielekeza katika kupunguza,”.
Pia amesema taasisi hiyo inatafuta mbinu za kuhakikisha upotevu wa samaki unaisha ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii.
“Samaki wanaomfikia mwananchi wa kawaida wengi ni dagaa, hivyo kuna upotevu mkubwa. Katika tafiti ambazo tumefanya tunaona kuna upotevu wa karibia asilimia 40. Ukivua kilo 100 maana yake kilo 40 inapotea.
“Sasa tunafanya nini? Sisi kama TAFIRI tunatafuta mbinu za kuhakikisha upotevu unaondoka lakini tunaelimisha jamii na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wametengeneza mkakati wa kufika mwaka 2030 wawe wamepunguza upoteevu huo,” amesema.