Na Mwandishi wetu
RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua Soko la Madini ya Vito na Dhahabu Wilayani Tunduru ikiwa ni moja ya shughuli alizofanya akiwa katika ziara ya kikazi ya siku sita Mkoani Ruvuma.
Katika uzinduzi huo Samia ameipongeza
Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa utekelezaji wa Sera ya kushirikiana na sekta binafsi kwa vitendo.
“Ni dhahiri kwamba ujenzi wa soko hili kubwa na la kisasa utarahisisha biashara ya madini Wilayani hapa na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji maduhuli ya Serikali sambamba na kudhibiti udanganyifu na utoroshaji wa madini”, amesema.

Pia Rais Samia amepongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali katika Mkoa wa Ruvuma ambapo alieleza kwamba kwa kipindi cha Julai na Agosti mwaka huu, zaidi ya Sh. Bilioni 6.5 zimekusanywa, hali inayoonyesha taswira nzuri ya makusanyo kadri muda unavyoendelea.
Vile vile Rais Samia amesisitiza kutambua mchango wa wachimbaji wadogo katika uchumi wa Taifa, na kumwelekeza Waziri wa Madini kuhakikisha STAMICO inawasimamia ipasavyo kuwaendeleza ili wanufaike na rasilimali hiyo.
Naye Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema mwaka wa fedha uliopita sekta ya madini ilikusanya na kuchangia kwenye mfuko mkuu wa Serikali Sh. Bilioni 753 ilhali kwa mwaka 2015/2016 Sh. Bilioni 161 pekee zilikusanywa.
“Maelekezo yako Rais ndiyo yamepelekea kwa mwaka 2023/2024 zaidi ya Sh. Trilioni 1.7 zizunguke kwenye masoko 43 na vituo vya ununuzi 102 nchi nzima kwenye biashara ya madini.
“Pamoja na mzunguko huo, sekta ya madini inaendelea kukua kwa kasi na kuchangia ukuaji wa vipato vya wananchi katika maeneo mbalimbali.
“Katika kipindi cha siku 84 za mwaka huu wa fedha yaani 2024/2025 tayari sekta ya madini imekusanya jumla ya Sh. Bilioni 225 na kuchangia katika mfuko mkuu wa Serikali, hii ni hatua kubwa katika maendeleo ya sekta ya madini na ukuaji wa uchumi wa Taifa letu” amesema.