Na Waandishi Wetu
KATIKA Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing (BFSU), kuna mwalimu wa siku nyingi ajulikanaye kama Shen Zhiying.
Mwalimu huyu aliweka jiwe la msingi katika kazi ya elimu ya lugha ya Kiswahili nchini China iliyoanzia mwaka 1960.
Alizaliwa Mjini Shanghai Mwaka 1934, Mwalimu huyo. Hivyo baada ya kuasisiwa kwa Jamhuri ya Watu wa China, yaani China Mpya, ujenzi wa nchi uliendelea.
Mwaka 1958, Shen alifanya uamuzi wa kujiunga na ujenzi wa diplomasia wa nchi mpya. Alipita mtihani akaingia Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing, akaanza kujifunza Kiingereza, akitumai kutoa mchango katika kazi ya ushirikiano na nchi za nje katika siku za mbele.
Mwaka wa 1960 ulikuwa mwaka wa uhuru kwa bara la Afrika ambapo nchi nyingi za Afrika ziling’oa kabisa ukoloni na kuanza ujenzi wa nchi mpya.
Nchi hizi zilitaka kuzidisha mawasiliano na ushirikiano na nchi nyingine, zikiwemo China. Mwaka huo huo, Hayati Waziri Mkuu wa China Zhou Enlai alitoa idhini ya kuanzisha kozi kadhaa mpya katika Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing, ikiwemo lugha ya Kiswahili.
Mwaka 1961, Kitivo cha Asia na Afrika kiliasisiwa rasmi. Shen Zhiying alichaguliwa na chuo kikuu kuwa mmojawapo katika wanafunzi wa kwanza waliojifunza Kiswahili.
Kusoma lugha mpya kulikuwa jambo gumu sana, sembuse kujifunza bila ya walimu, vitabu wala kamusi kutokana na hali halisi.
Wanafunzi wa Kiswahili walikuwa na kamusi moja tu – ya Kirusi-Kiswahili. Kwa hivyo, iliwabidi watafsiri kamusi hiyo kwa lugha ya Kichina, ili waendelee kujifunza.
Walisikiliza idhaa ya Kiswahili iliweza kuwasaidia wanafunzi kujifunza Kiswahili.
Lakini idhaa nyingi za Kiswahili zilikuwa za India, Uingereza na Marekani. Tofauti ya nyakati iliwapasa wanafunzi hao kukesha ili waweze kurekodi idhaa hizo kwa madhumuni ya kujifunza lugha.
Kuna methali isemayo ‘Mchumia juani hulia kivulini’ hivyo Mchakato wa kujifunza Kiswahili ulikuwa ngumu, lakini pia ni muhimu tena yenye faida.
Desemba 1986, wajumbe wa China walioongozwa na Shen Zhiying walihudhuria Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Kiswahili kwenye Zanzibar
Mwalimu Shen aliwahi kusema, ‘Kazi yetu tilipewa na nchi, hivyo ni jukumu letu kujifunza vizuri na hatimaye kucharaza lugha hii ya Kiswahili’.
Mwaka 1963, Shen alihitimu na kuanza kuwafundisha wanafunzi wa China lugha ya Kiswahili.Vilevile alibeba jukumu la kufanya kazi za ukalimani kwa viongozi wa taifa.
Miaka ya 1960 na 1970, Shen alikuwa mkalimani kwa viongozi mbalimbali wa China, wakiwemo Hayati Mwenyekiti Mao Zedong, Hayati Mwenyekiti Liu Shaoqi, Hayati Waziri Mkuu Zhou Enlai, Hayati Katibu Mkuu Zhu De, na Hayati Waziri Chen Yi. Ameshuhudia urafiki baina ya China na Afrika. Ziara nchini Tanzania pamoja na Waziri Mkuu Zhou Enlai ilimpa Shen kumbukumbu isiyosahaulika.
Julai 24, 1965, Hayati Mwenyekiti Mao Zedong alipokutana na Ujumbe wa Wanawake wa Tanzania ulioongozwa na Mke wa Rais Karume wa Zanzibar, Shen Zhiying alikuwa mkalimani.
Mwaka 1965, Hayati Waziri Mkuu Zhou Enlai alifanya ziara nchini Tanzania. Baada ya kufika Dar es Salaam, mkutano wa kukaribisha ujumbe wa China ulifanyika kwenye uwanja wa michezo.
Waziri Mkuu Zhou alitoa hotuba na Shen alikuwa mkalimani wake. Wakati watu wa Tanzania waliposikia hotuba yake kwa lugha yao wenyewe – Kiswahili, walishangilia sana! Wengine walipiga filimbi, walicheza ngoma, walirusha juu kofia na nguo… Wakipiga yowe “China! China! Zhou Enlai! Zhou Enlai!”
Hotuba ilikatika na shangilio la watu mara nyingi. Rais Nyerere alisema, “Hapo zamani, haikuwa hata mara moja kwamba hotuba ya kiongozi wa nchi nyingine iliweza kuwasisimua watu namna hii. Sababu zilikuwa mbili: Hotuba yenyewe ilikuwa nzuri kabisa, ambayo ilituhamasisha kupinga ubeberu na ukoloni, na kutusaidia kujenga nchi yetu;
Ya pili, hotuba ilitafsiriwa kwa Kiswahili, ambayo kila Mtanzania anaweza kuelewa. Mioyo yetu inakuwa karibu zaidi kwa sababu ya lugha.”
Juni 1965, Hayati Waziri Mkuu Zhou Enlai alipofanya mazungumzo na Rais Karume wa Zanzibar wakati wa ziara yake nchini Tanzania, Shen Zhiying alikuwa mkalimani
Hapo zamani, kutumia Kiingereza au lugha nyingine kubwa kulikuwa jadi ya mazungumzo ya diplomasia. Baada ya hapo, Waziri Mkuu Zhou aliamua kutumia Kiswahili wala si Kiingereza wakati wa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Tanzania. Shen akabahatika kujionea ujenzi wa urafiki kati ya China na Afrika. “Kweli, ni fahari yangu kubwa.” Alisema.
Ifikapo miaka ya 1980, maendeleo ya ufundishaji wa lugha na utamaduni wa kigeni nchini China yaliingia “zama za dhahabu”, Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing kimekuwa kwenye mstari wa mbele wa kukuza uelewano na ushirikiano baina ya China na dunia.
Hivyo Mwaka 2019 Kitivo cha Lugha za Afrika kilianzishwa, kinasomesha lugha 20 za Afrika, jambo ambalo limetoa mchango mkubwa kwa kuendeleza mawasiliano na ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika kwa njia ya kuwatayarisha vijana wenye ujuzi na uwezo. Wanafunzi wengi wa Kiswahili nchini China watapata nafasi ya kwenda nchi za Afrika ili kusoma na kutafiti lugha za Kiafrika na utamaduni wa Afrika.
Wachina husema: “Mwenye maadili hakosi marafiki.” Mchango mkubwa uliotolewa na Profesa Shen Zhiying kwa urafiki baina ya China na Afrika umekuwa mnara kubwa usiosahaulika.
Wanafunzi wa leo wataendeleza kazi hii muhimu iliyoanzishwa naye, wataendelea kuchukuana na kushirikiana na watu wa Afrika ili kukuza mawasiliano na uelewano kati ya China na Afrika.
Waandishi: Yu Minghong, Wei Yuanyuan, Chuo Kikuu cha Lugha za Kigeni cha Beijing (BFSU)