Na Danson Kaijage.
WAZIRI wa Nishati, Judith Kapinga amesema Serikali kupitia wizara hiyo imetumia Sh. Bilioni 107.36 kupeleka umeme kwenye Vijiji vyote 474 vya Mkoa wa Simiyu.

Kapinga ameyasema hayo wakati akitoa tathmini ya hali ya upatikanaji wa umeme Mkoa wa Simiyu na maendeleo ya usambazaji wa nishati safi ya kupikia wakati wa kuhitimisha ziara ya kikazi ya Rais, Samia Suluhu Hassan Mkoani humo.
“Mheshimiwa Rais baada ya kumaliza upelekaji wa umeme kwenye Vijiji, hivi sasa tunapeleka umeme kwenye Vitongoji na hivi sasa tunatekeleza miradi ya umeme kwenye Vitongoji 638 kati ya Vitongoji 1,408 vya Mkoa wa Simiyu”, amesema.
Amesema Serikali itajenga kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Simiyu kupitia mradi wa gridi imara, pia hivi sasa Mkoa huo unapata huduma ya umeme kutoka Mikoa mitatu ya Shinyanga, Mwanza na Mara.

Amesema kituo hicho kitazidi kuimarisha hali ya umeme Simiyu na hivyo kuwa muhimu kwa maendeleo ya watu wa Simiyu.
Amesema mradi wa gridi imara mkoani Simiyu una sehemu mbili ambazo ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Ibadakuli Shinyanga hadi Bariadi utakaojengwa kwa takribani Sh. Bilioni 48 na ujenzi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Bariadi kitakachojengwa kwa gharama ya Sh. Bilioni 49.
Amesema kukamilika kwa mradi wa kituo cha kupokea na kupoza umeme Mkoa wa Simiyu utawezesha Mkoa kuwa na uwezo wa megawati 150.
Kuhusu Nishati Safi ya Kupikia, Kapinga amesema Mkoa wa Simiyu umepata mitungi ya gesi ya ruzuku takribani 16,275 ambayo yote tayari imeshachukuliwa na wananchi kwa bei ya ruzuku.